Watu 164 wameuwawa, katika machafuko Kazakhstan
9 Januari 2022Taarifa hiyo ni kwa mujibu wa shirikal la habari la Sputnik la Urusi. Watoto wawili ni miongoni mwa waliouwawa kwenye machafuko hayo. Kati ya 164 waliouwawa, 103 kati yao ni kutoka katika mji wa Almaty.
Katika machafuko hayo pia, zaidi ya watu 5,000 wamekamatwa na mamlaka za nchi hiyo. Ni katika maandamano yaliyotikisa taifa hilo kubwa zaidi la Asia ya kati wiki iliyopita. Taarifa za idadi ya vifo na waliokamatwa imetolewa leo Jumapili. Idadi ya waliokamatwa inaifanya jumla ya wanaoshikiliwa kwa mahojiano kutokana na maandamano hayo kufikia 5,135.
Taifa hilo lenye takribani raia milioni 19 na utajiri mkubwa wa nishati, limegubikwa na maandamano kwa wiki moja sasa, huku watu kadhaa wakiuwawa.
Kupanda kwa bei ya mafuta ndiko kulikosababisha machafuko katika mikoa ya magharibi mwa taifa hilo. Machafuko hayo yalisambaa hadi kwenye miji mikubwa ukiwemo mji muhimu wa kibashara wa Almaty ambako maandamano yaliibuka na polisi walitumia risasi za moto kuwatawanya waandamanaji.
Vurugu zimesababisha uharibifu mkubwa
Akizungumzia hasara iliyotokana na machafuko mapema leo, waziri wa mambo ya ndani wa Kazakhstan, Erlan Turgumbayev amesema makadirio ya awali ya mali zilizoharibiwa ni karibu Euro milioni 155 sawa na dola za kimarekani milioni 198.
Waziri huyo wa mambo ya ndani wa nchi hiyo amenukuliwa akisema kuwa, zaidi ya biashara 100 na benki kadhaa zilivamiwa na kuporwa katika machafuko hayo huku takribani magari 400 yakiharibiwa.
Hata hivyo ameongeza kuwa kwa sasa hali imetengamaa katika maeneo mengi ya Kazakhstan lakini operesheni ya kupambana na kile alichokiita ugaidi inaendelea ili kurejesha utulivu. Kwa sasa, hali nchini humo inaonekana kuwa ya utulivu katika mji wa Almaty ingawa wakati mwingine polisi wamekuwa wakirusha risasi hewani ili kuwazuia watu kukaribia uwanja mkubwa ulio katikati mwa mji huo.