1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 16 wauawa katika mapigano Somalia

27 Januari 2010

Mapigano hayo yametokea leo kati ya kundi la wanamgambo wanaoiunga mkono serikali ya mpito ya Somalia na makundi mawili ya waasi.

https://p.dw.com/p/LiBU
Miili ya watu waliouawa katika mapigano nchini Somalia.Picha: AP

Watu 16 wameuawa nchini Somalia na wengine 34 wamejeruhiwa baada ya kuzuka mapigano kati ya wanamgambo wanaoiunga mkono serikali ya mpito ya nchi hiyo na waasi wa Kiislamu.

Mapigano hayo yaliyosababisha mauaji yametokea leo kati kati ya mkoa wa Galgadug. Makamu mwenyekiti wa shirika la kutetea amani na haki za binadamu mjini Mogadishu la Elman, Ali Yasin Gedi ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa watu wengine zaidi walilazimika kuyakimbia makaazi yao. Wakaazi wa mkoa huo wamesema kuwa mapigano hayo yametokea katika miji ya Warhole na Owsweyne kati ya kundi lisilo na msimamo mkali wa kidini la Ahlu Sunna Waljamaca dhidi ya kundi la Hizbul Islam na wapiganaji wa al-Shabaab.

Marekani inasema kuwa kundi la al-shabaab ambalo lina mafungamano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda liko nchini Somalia kwa niaba ya mtandao huo wa kigaidi. Makundi yote ya Hizbul Islam na al-Shabaab yanataka kutumika kwa sheria ya kiislamu ya Sharia katika nchi hiyo inayokabiliwa na mapigano ya mara kwa mara.

Bashir Khayre, mkaazi wa Warhole ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba raia watatu wamekufa kutokana na majeraha waliyoyapata wakati majirani zao walipokuwa wakijaribu kukimbia nao kwa ajili ya kwenda kutafuta usalama zaidi wa maisha yao katika mji mwingine. Khayre amesema mapigano hayo kwa sasa yamesimama, lakini inasemekana mapigano hayo huenda yakaanza tena kwa sababu makundi hayo mawili yako katika maeneo ya karibu. Hata hivyo idadi ya watu waliouawa katika mapigano hayo huenda ikaongezeka.

Wapiganaji wa Hizbul Islam na al-Shabaab wamekuwa wakipigana wenyewe kwa wenyewe, lakini wakati mwingine huwa wanaungana pamoja kwa ajili ya kupambana na kundi la Ahlu Sunna Waljamaca ambalo halina msimamo mkali wa kidini na linaiunga mkono serikali ya mpito ya Rais Sheikh Sherif Ahmed inayoungwa mkono na mataifa ya Magharibi.

Wakati huo huo, jana Jumanne watu wengine wanane waliuawa katika mapigano yaliyotokea kwenye mji wa Beledweyne. Aidha, siku ya jumatatu kundi la al-Shabaab liliishambulia kambi ya vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Afrika nchini Somalia, katika mji mkuu wa nchi hiyo, Mogadishu. Shambulio hilo lilitokea katika eneo la hospitali ambako raia wa kawaida pia walikuwa wakipatiwa matibabu.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (RTRE/AFPE)

Mhariri: Othman Miraji