Watu 13 wauawa katika siku ya kwanza ya maandamano Nigeria
2 Agosti 2024Mamlaka nchini Nigeria zimethibitisha kuuawa kwa watu wanne kutokana na shambulizi la bomu na kukamatwa kwa mamia ya waandamanaji, hatua iliyochochea marufuku ya kutotoka nje katika majimbo kadhaa.
Soma pia:Polisi Nigeria wafyatua gesi ya machozi kutawanya waandamanaji
Katika mahojiano, mkurugenzi wa Amnesty International nchini Nigeria, Isa Sanusi, amesema shirika hilo lilithibitisha kwa njia huru mauaji hayo ambayo yaliripotiwa na mashuhuda, familia za waathiriwa pamoja na mawakili.
Marufuku ya kutotoka nje yawekwa katika majimbo kadhaa
Polisi nchini humo imesema kuwa zaidi ya waandamanaji 300 walikamatwa na marufuku ya kutotoka nje kuwekwa katika majimbo ya Kaskazini ya Kano na Katsina baada ya kuporwa kwa mali ya serikali na umma.
Afisa mmoja wa polisi pia aliuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa.
Maandamano hayo zaidi yalikuwa juu ya uhaba wa chakula na madai ya utawala mbaya nchini humo.
Maafisa wa umma nchini Nigeria ni miongoni mwa wanaolipwa vizuri barani Afrika
Maafisa wa umma nchini Nigeria, ambao mara kwa mara wanatuhumiwa kwa ufisadi, ni miongoni mwa maafisa wanaolipwa vizuri zaidi baraniAfrika, hii ikiwa tofauti kubwa katika taifa hilo ambalo lina watu maskini zaidi duniani licha ya kuwa moja ya mataifa yenye utajiri mkubwa wa mafuta barani Afrika.
Waandamanaji wanataka kurejeshwa kwa ruzuku ya gesi
Siku ya Alhamisi wakiwa wamebeba mabango, kengele na bendera ya Nigeria ya rangi za kijani na nyeupe, waandamanaji waliimba nyimbo huku wakiorodhesha matakwa yao.
Waandamanajihao pia wanataka kurejeshwa kwa ruzuku ya gesi na umeme ambayo kuondolewa kwake kama sehemu ya mageuzi ya serikali ya kukuza uchumi kumesababisha mfumuko mkubwa wa bei na kushuka kwa thamani ya Naira.