1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

Watu 13 wadaiwa kuuawa na kundi la RSF

4 Novemba 2024

Takriban watu 13 wameuawa kwa kupigwa risasi jana Jumapili katika shambulizi linalodaiwa kufanywa na kundi la wanamgambo la RSF katika jimbo la Al-Jazira kusini mwa Khartoum nchini Sudan.

https://p.dw.com/p/4mZgn
Mizozo | Bendera ya Sudan ikiwa juu ya mtutu wa bunduki
Bendera ya Sudan ikiwa juu ya mtutu wa bundukiPicha: Umit Bektas/REUTERS

Haya ni kwa mujibu wa chanzo kimoja cha matibabu kilicholiarifu shirika la habari la AFP.

Chanzo hicho kilichozungumza kwa sharti la kutotajwa jina, kimesema kikosi hicho cha RSF kiliwafyetulia risasi watu hao katika mji wa Al-Hilaliya.

Jimbo la Al-Jazira nchini Sudan limekuwa kitovu cha mapigano tangu kamanda wa RSF, Abu Aqla Kaykal, alipotangaza kuliasi kundi hilo na kujiunga na upande hasimu wa jeshi la taifa.

Soma pia:Mpango wa Chakula, WFP waomba utulivu nchini Sudan ili litoe huduma zake

Kulingana na mratibu wa misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan, Clementine Nkweta-Salami, RSF ilianzisha mashambulizi makubwa katika maeneo ya mashariki ya jimbo la Al-Jazira kati ya Oktoba 20 na 25. 

Afisa huyo amesema wanamgambo hao wanatuhumiwa kufanya mauaji ya halaiki, vitendo vya unyanyasaji watu kingono, uporaji mali kwenye masoko na majumba pamoja na kuchoma moto mashamba.