1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 120 wauwawa kwenye mashambulio ya angani nchini Irak

8 Desemba 2016

Mashambulio hayo yametokea katika mji wa Qaim unaoshikiliwa na wapiganaji wa IS nchini Irak. Watu wengine 170 wamejeruhiwa katika mashambulizi hayo katika eneo la magharibi mwa Irak karibu na mpaka wa Syria.

https://p.dw.com/p/2TyNr
Kampf um Mossul
Picha: picture-alliance/dpa/A. Jalil

Spika wa bunge la Irak, Salim al-Jabouri amesema kwamba serikali ya Irak inapaswa kubeba dhamana ya makosa hayo yaliyotokea na vile vile ianzishe uchunguzi utakaobaini ukweli wa mauaji hayo, na  wakati huo huo ameitaka serikali iwahakikishie raia kuwa tukio kama hilo linalo walenga raia moja kwa moja halitatokea tena.

Mashambulio hayo yalilenga katika eneo la soko kwenye mji huo wa Qaim ulioko Magharibi mwa nchi, takriban kilomita 500 kutoka mji mkuu wa Baghdad. Mbunge Fares al Fares ameeleza kwamba ndege za Irak zilifanya mashambulio hayo ingawa hakutoa maelezo zaidi. Hali kadhalika, hadi sasa serikali haijatoa tamko lolote kuhusiana na mashamabulizi hayo. Mnamo miezi ya hivi karibuni vikosi vya Irak vinavyoungwa mkono na Marekani vimekuwa vikiendeleza mashambulio dhidi ya wapiganaji wa IS ambao waliyanyakua maeneo mengi katika mashambulizi yenye kasi kubwa mnamo mwaka 2014.

Duru za hospitali pamoja na baadhi ya wabunge zinaelezea juu ya kutokea mashambulio matatu ya angani katika mji huo wa Qaim.  Msemaji wa kikosi kinachoongozwa na Marekani kinachoshirikiana na majeshi ya Irak katika mapambano dhidi ya IS amekanusha kuwa wamehusika na mashambulio hayo ya angani ambayo kitengo cha habari cha IS kinaelekeza lawama kwa vikosi vya kijeshi vya serikali.

Salim al-Jubouri neuer Parlamentspräsident von Irak Archiv 2010
Salim al-Jabouri Spika wa bunge la IrakPicha: picture alliance/AP Photo

Salim al-Jabouri mwanasiasa mashuhuri wa Kisunni na wa ngazi ya juu katika siasa za Irak, amesema mashambulio hayo yalilenga kimakusudi katika maeneo ya raia kwa mfano maduka ndio maana watu wengi wameuwawa na wengine wengi wamejeruhiwa. Kwa kiwango kikubwa nchi ya Irak inaongozwa na wanasiasa wa Kishia, mji wa Qaim na eneo lote la mkoa wa magharibi ni sehemu ambayo ina Wassuni wengi na pia bado inashikiliwa na kundi la IS.  Mashambulio hayo yametokea wakati ambapo majeshi ya serikali ya Irak yanaendeleza kampeni yake ya wiki saba yenye lengo la kuwaangamiza wapiganaji wa IS ambao pia wameuteka mji wa Mosul ulio takriban kilomita 280 kaskazini mashariki mwa mji huo wa Qaim.

Katika siku za hivi karibuni wapiganaji wa IS wameshindwa vibaya katika mapigano katika mji wa Mosul nchini Irak na pia katika mji wa Aleppo nchini Syria.

Mwandishi: Zainab Aziz/RTRE/DPAE

Mhariri: Gakuba Daniel