1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 12 wauwawa wanne wakombolewa Mali

10 Agosti 2015

Watu 12 wameuwawa baada ya vikosi vya usalama nchini Mali Jumamosi (08.08.2015) kuivamia hoteli inayotumiwa na wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa, na kuwakombowa mateka wanne waliokuwa wakishikiliwa na wanamgambo.

https://p.dw.com/p/1GC8U
Kikosi cha jeshi la serikali Mali.
Kikosi cha jeshi la serikali Mali.Picha: Reuters

Wanamgambo hao wa Kiislamu wa itikadi kali waliiteka hoteli ya Byblos ilioko katika mji wa Sevare, kilomita 600 kaskazini mashariki ya mji mkuu wa nchi hiyo ya Afrika Magharibi wa Bamako mapema Ijumaa. Na kuvizuwiya vikosi vya serikali vilivyowazingira visiikaribie hoteli hiyo.

Shambulio hilo ambalo limetokea mbali kabisa na eneo la kusini la jangwani ambayo ni ngome kuu ya wanamgambo wa Kiislamu wa itikadi kali, ni la karibuni kabisa katika kile kinachoonekana kuwa kuongezeka kwa mashambulizi dhidi ya wanajeshi wa Mali na wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa. Mashambulizi hayo yanayofanywa na mabaki ya waasi, wenye mafungamano na kundi la Al Qaeda.

Msemaji wa wizara ya ulinzi ya Mali Kanali Diaran Kone, amesema kuzingirwa kwa hoteli hiyo kumemalizika vizuri na kuwakombowa mateka wanne. Lakini kwa bahati mbaya pia, wamegunduwa maiti tatu kwenye hoteli hiyo.

Msemaji wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini Mali MINUSMA amesema, wafanyakazi wanne wa Umoja wa Mataifa wawili kutoka Afrika Kusini, Mrusi mmoja pamoja na Muukraine mmoja wamekombolewa katika shambulio lililofanywa na vikosi vya usalama kabla ya alfajiri.

Rai waliouwawa

Radhia Achouri amesema magaidi hawakuwahi kuwagunduwa wafanyakazi hao hotelini, na kwamba wanachunguza iwapo kuna wafanyakazi wengine wa MINUSMA waliokuwepo kwenye hoteli hiyo.

Kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini Mali MINUSMA.
Kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini Mali MINUSMA.Picha: Reuters

Kwa mujibu wa msemaji wa serikali ya Mali Choguel Kokala Maiga, mateka watatu waliuwawa wakati wa prukushani hiyo na wanatoka Afrika Kusini,Urusi na Ukraine. Wizara ya mambo ya nje ya Afrika Kusini imethibitisha kwamba raia wake wawili wako salama, wakati mkaazi wa Pretoria mwenye umri wa miaka 38 aliyeajiriwa na kikosi cha MINUSMA kutoka kampuni ya masuala ya anga amefariki.

Amesema, wanajeshi watano na wanamgambo wanne akiwemo yule ambaye awali ilisemekana alikuwa amevalia ukanda wa miripuko pia wameuwawa.

Awali Urusi na Ukraine zilithibitisha kwamba, raia wake walikuwa miongoni mwa mateka waliokuwa wakishikiliwa kwenye hoteli hiyo.

Watuhumiwa saba mbaroni

Taarifa ya serikali iliyotolewa baadae hapo Ijumaa, imesema watuhumiwa saba wamekamatwa kuhusiana na shambulio hilo.

Mazungumzo ya kutafuta amani Mali yaliokuwa yakifanyika Algeia.
Mazungumzo ya kutafuta amani Mali yaliokuwa yakifanyika Algeia.Picha: Farouk Batiche/AFP/Getty Images

Operesheni ya kijeshi iliyoongozwa na Ufaransa hapo mwaka 2013, iliwatimuwa wapiganaji wengi wa Kiislamu wa itikadi kali. Ambao walikuwa wametumia kwa faida yao uasi wa kabila la Tuareg na mapinduzi ya kijeshi, kunyakuwa maeneo ya kaskazini mwaka mmoja kabla.

Wakati Umoja wa Mataifa umeweza kufankisha makubaliano dhaifu kati ya serikali na waasi wa Tuareg wanaotaka kujitenga, wapiganaji wa Kiislamu wa itikadi kali ambao hawakujumuishwa kwenye mazungumzo hayo wamekuwa wakiendeleza harakati za uasi.

Hapo Ijumaa vikosi vya usalama vya Mali vilitumia silaha nzito yakiwemo maguruneti yanayovurumishwa kwa roketi, kujaribu kuwachopowa bila ya mafanikio wanamgambo hao. Operesheni hiyo ilifanyika hotelini, na kudumu kwa takriban saa 24.

Wanajeshi wa Ufaransa wanatajwa kukisaidia kikosi maalum cha Mali katika operesheni hiyo, lakini jeshi la Ufaransa limesema halikuhusika moja kwa moja na kwamba dhima iliyotimiza ni ile ya uratibu ambayo ni ya kawaida kwa wakati huu.

Mwandishi : Mohamed Dahman /Reuters

Mhariri : Elizabeth Shoo