1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 12 wafa kwa kirusi cha corona Iran, 80,000 duniani kote

24 Februari 2020

Khofu ya virusi vya corona inazidi kuwa kubwa baada ya kupanda kwa maambukizi mapya nchini Iran, Italia na Korea Kusini, ingawa kiwango cha maambukizi mapya kimeshuka ndani ya China, kuliko chimbuko la kirusi hicho.

https://p.dw.com/p/3YGz3
Italien Coronavirus Codogno
Picha: Reuters/F. Lo Scalzo

Mkoa wa nne wa ukubwa nchini Korea Kusini, Daegu, umeongeza marufuku yake ya kuingia na kutoka, huku idadi ya maambukizi mapya ikipanda juu kwa kasi. Mashirika ya ndege ya Asian Airlines na Korean Air yamesitisha safari kwenye mji huo hadi tarehe 9 na 28 mwezi ujao wa Machi.

Waziri wa Afya wa Korea Kusini, Kim Kang-lip, amesema endapo watashindwa kuzuwia kusambaa kwa kirusi hicho kwenye mkoa wa Daegu, kuna uwezekano wa kusambaa nchi nzima. Hadi sasa, amesema waziri huyo, zaidi ya watu 700 nchini humo wameshaambukizwa.

"Kufikia leo, idadi ya wagonjwa walioambukizwa kirusi cha corona imefikia 763. Miongoni mwao, 18 wamepona kabisa na wameruhusiwa kurudi nyumbani na saba wamefariki dunia. Wengi wa walioambukiwa wamepatikana kwenye Kanisa la Shincheonji mkoani Daegu na kwenye Hospitali ya Daenam mjinji Cheongdo," alisema waziri huyo.

Ligi ya soka imeahirishwa kwa muda usiojulikana kote Korea Kusini kwa hofu ya kirusi cha corona.

Watu 4 wafa Italia, 12 Iran, Ulaya na Asia zachukuwa tahadhari

Barani Ulaya, Waziri wa Afya wa Ufaransa Olivier Veran amesema atakutana na wenzake wa Umoja wa Ulaya hivi karibuni kujadiliana njia za kukabiliana na uwezekano wa kusambaa kwa kirusi hicho barani humu. Hayo yanakuja wakati Italia ikithibitisha kifo cha mtu mwengine wa nne, na maambukizi ya wengine 150.

Afghanistan Coronavirus Flughafen Kabul
Hatua za udhibiti wa kirusi cha corona kwenye uwanja wa ndege wa Kabul, Afghanistan.Picha: picture-alliance/dpa/R. Gul

Maambukizi yameripotiwa katika mataifa ya Ghuba na Mashariki ya Kati, ambapo Iran imethibitisha vifo vya watu 12 hadi sasa na wengine 43 wakiwa wameshaambukizwa. Bahrain imeripoti mgonjwa wake wa kwanza na Kuwait imesema watu watatu waliowahi kutembelea Iran wamegunduliwa na kirusi hicho. Maambukizi mengi nchini Iran yamegunduliwa kwenye mji mtukufu kwa waumini wa madhehebu ya Shia, Qom.

Saudi Arabia, Kuwait, Iraq, Uturuki na Afghanistan zimeweka masharti magumu kwa watu kuingia na kutoka Iran kupitia mipaka yao. 

Hadi kufikia jana jioni, Japan ilikuwa na wagonjwa 773, wengi wao wakiwa wale walio kwenye meli iliyowekewa karantini karibu na mji mkuu, Tokyo, ambako abiria wa tatu, mzee wa miaka 80 raia wa Japan, alikufa kwa kirusi hicho.

China Bara, ambako ndiko chimbuko la kirusi cha corona, imeripoti wagonjwa wapya 409, kutoka kiwango cha wagonjwa 648 kwa siku. Hii inawafanya wagonjwa walioambukizwa kufikia 77,150 ambapo idadi ya walipoteza maisha imepanda hadi 2,592 kwa China Bara pekee.