Watu 11 wauawa Somalia
4 Februari 2019Kiasi ya watu 11 wameuawa baada ya shambulizi kutokea karibu na eneo la maduka makubwa mjini Mogadishu. Afisa wa Polisi, Ahmed Baashane amesema kuwa mripuko huo ulisababishwa na bomu lililokuwa limetegwa kwenye gari katika eneo la kuegeshea magari, lakini haijafahamika wazi iwapo mtu aliyejitoa mhanga anahusika.
Kwa mujibu wa afisa mwingine wa polisi, Ali Hassan Kulmiye, zaidi ya watu 15 wamejeruhiwa na wanapatiwa matibabu hospitali. Mtandao unaowaunga mkono wapiganaji wa Al-Shabaab, somalimemo.net, umemnukuu afisa wa wa Al-Shabaa ambaye hakutajwa jina, akidai kundi hilo linahusika na shambulizi hilo.
Afisa huyo amesema walikuwa wakiwalenga maafisa wa serikali waliokuwa wanakutana kwenye mgahawa mmoja karibu na eneo hilo la maduka. Mara kwa mara kundi hilo limekuwa likifanya mashambulizi kwenye majengo ya serikali, hoteli na migahawa kwenye taifa hilo la Pembe ya Afrika linalokabiliwa na mashambulizi.
Al-Shabaab lina mafungamano na mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda.