Watu 11 wauawa kwenye mapigano mapya Kenya
16 Machi 2017Miongoni mwa waliouawa katika mapigano mapya yaliyozuka wiki hii kati ya jamii ya Pokot na Ilchamus ni pamoja na watoto watatu na wanawake saba. Mapigano hayo yamezuka wiki mbili baada ya Shirika la Msalaba Mwekundu nchini humo kusimamisha shughuli zake kwa kuhofia usalama wa maafisa wake.
Mapigano mapya yamezuka katika Kaunti ya Baringo licha ya kikosi cha maafisa wa usalama wapatao 2,000 kupelekwa katika eneo hilo wiki mbili zilizopita. Wakazi wa eneo hilo wameitaka serikali kuimarisha usalama.
Mapigano hayo yamezuka huku Rais Rais Uhuru Kenyatta akitoa Onyo kwa wanasiasa wanaochochea ghasia katika eneo la Bonde la Ufa. Rais Kenyatta alisema, ninanukuu ''tutatumia mbinu zote tulizonazo kuwaweka katika mkono wa sheria wote wanaohusika kuchochea mapigano hayo na nachukua fursa hii kuwaonya wanasiasa katika maeneo yaliyoathiriwa kukoma kuchochea mapigano ya aina yoyote kwani mtakabiliwa kisheria''.
Tayari watatu wametiwa mbaroni kuhusiana na mauaji hayo yaliyotokea usiku wa kuamkia jana. Shirika la Msalaba Mwekundu nchini Kenya ambalo wiki mbili zilizopita lilisimamisha shughuli zake za kusambaza misaada ya kiutu limeomba serikali kuu kutoa ulinzi kwa maafisa wake ili wasije wakashambuliwa tena wiki moja baada ya kurejea katika shughuli hizo.
Serikali imeorodhesha eneo la Baringo kuwa eneo hatari na kupeleka kikosi cha zaidi ya maafisa 2,000 wa usalama kuzima aina yoyote ya ghasia. Licha ya kikosi hicho cha usalama kupelekwa eneo hilo jamii zinazozozana bado zimeendeleza uhasama na kufanya mashambulizi tena.
Eneo la Baringo limekuwa likikumbwa na ghasia hasa kila wakati uchaguzi unapokaribia. Wanasiasa wa eneo hilo wamelaumiwa kwa kuchochea ghasia.
Mwandishi: Alfred Kiti
Mhariri: Saumu Yusuf