Watu 10 wachinjwa Msumbiji
30 Mei 2018Vijana wawili wa kiume ni miongoni mwa wale waliokatwa shingo zao siku ya Jumapili, msemaji wa polisi ya Msumbiji Inacio Dina aliwaambia waandishi habari , na kuongeza kwamba polisi sasa wameanzisha msako kuwatafuta waliohusika. Dina alithibitisha kwamba kuna watu kutoka nje ya nchi pamoja na raia wa Msumbiji katika kundi hilo la washambuliaji.
"Hili ni kundi ambalo kwa kiasi kikubwa ni dhaifu. Kile tulichokishuhudia ni kukata tamaa kwa kiasi kikubwa kwa kundi hili kwa kujaribu baadhi ya viongozi wa kundi hili kufanya uhalifu huu wa kinyama."
Hakuna mtu ambaye amekwisha kamatwa hadi sasa kwa mujibu wa msemaji huyo wa polisi Inacio Dina. Hata hivyo hakutaka kukihusisha kitendo hicho na kundi ambalo liliwauwa zaidi ya watu 20 katika jimbo la Cabo Delgado mwezi Oktoba, ama iwapo kuna uhusiano na kundi la Waislamu wenye itikadi kali. Ripoti kutoka katika eneo hilo zinazungumzia kwamba washambuliaji wana mahusano na makundi ya itikadi kali ya Kiislamu.
Msumbiji ambayo kwa kiasi kikubwa ina waumini wengi wa Kikristo , katika pwani ya kusini mashariki mwa bara la Afrika hakujakuwa na makundi ya waislamu wenye itikadi kali hapo kabla.
al-Shabaab Msumbiji
Mapema mwaka huu , taarifa moja katika tovuti ya kituo cha kukusanya mawazo kilicho na makao yake makuu nchini Marekani cha Kituo cha Afrika cha mitaala ya mikakati kimesema shambulio la Oktoba , liliwapata "wachunguzi wa mapambano ya wapiganaji wa kimataifa wa jihadi kwa mshangao."
Hata hivyo , taarifa hiyo ilisema , kundi "linalofahamika ndani ya nchi hiyo kama al-Shabaab na Swahili Sunnah yanaonekana kuwavutia watu wapya wa kulitumikia kundi hilo" nchini Msumbuji.
Bila ya kutaja kundi hilo la washambuliaji kwa jina, msemaji wa polisi Dina aliapa kwamba watawasaka na kuwakamata watu wote waliohusika na kitendo hicho na kuwafikisha mahakamani.
"Kile kinachofanyika ni kuwasaka wale waliohusika na kuwafikisha kizuwizini na kuwawajibisha kwa njia ya sheria kama wengi wengine ambao tayari wamefikishwa mbele ya sheria na kuwajibishwa."
Jimbo la Cabo Delgado limeshuhudia mashambulizi kadhaa yaliyofanywa na wanaoshukiwa kuwa Waislamu wenye itikadi kali tangu mwezi Oktoba mwaka jana. Mmoja kati ya wahanga katika shambulio la hivi karibuni alikuwa kiongozi wa kijiji cha Monjane, mkaazi wa eneo hilo , bila ya kutaja jina lake kwa hofu ya kulipiziwa kisasi.
Walimshambulia kiongozi huyo kwa kuwa alikuwa anatoa taarifa kwa polisi juu ya maeneo ambayo kundi la al-Shabaab liko katika msitu, aliliambia shirika la habari la afp , akimaanisha kundi lenye silaha linaloaminika kuhusika na shambulio la mwezi Oktoba katika kituo cha polisi na kituo cha upekuzi cha kijeshi katika mji wa Mocimboa da Praia.
Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Grace Patricia Kabogo