1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watoto wa Mubarak waachwa huru Misri

26 Januari 2015

Watoto wawili wa kiume wa Rais aliyeondolewa madarakani wa Misri Hosni Mubarak Jumatatu (26.01.2015) wameachiliwa huru kutoka gerezani takriban miaka minne baada ya kukamatwa kwa mara ya kwanza pamoja na baba yao

https://p.dw.com/p/1EQhQ
Rais wa zamani wa Misri Hosni Mubarak(katikati) na watoto wake wakati wa kusikilizwa kwa mojawapo ya kesi zao mjini Cairo ,Gamal(kushoto) na Alaa (kulia).
Rais wa zamani wa Misri Hosni Mubarak(katikati) na watoto wake wakati wa kusikilizwa kwa mojawapo ya kesi zao mjini Cairo ,Gamal(kushoto) na Alaa (kulia).Picha: Ahmed El-Malky/AFP/Getty Images

Maafisa wa usalama wamesema watoto hao ambao ni wafanyabiashara matajiri Alaa na Gamal ambaye wakati fulani alionekana ndie atakayerithi nafasi ya baba yake katika wadhifa wa urais, waliachiwa huru kutoka gereza la Torah lilioko kitongoji cha kusini mwa Cairo muda mfupi baada ya mapumziko mafupi ya shughuli za mchana na moja kwa moja kuelekea kwenye nyumba zao zilioko katika kitongoji cha kitajiri cha Heliopolis mjini Cairo.

Watoto hao pamoja na baba yao bado wanakabiliwa na kesi itakayosikilizwa upya kuhusiana na rushwa. Katika kesi nyengine tafauti watoto hao wanakabiliwa na kesi nyengine tafauti ya madai ya kuvujisha siri za biashara lakini wameonekana hawana hatia kwa mashtaka mengine.

Mubarak mwenye umri wa miaka 86 na mgonjwa alijiuzulu mwezi wa Februari mwaka 2011 kutokana na uasi wa umma na alikamatwa pamoja na watoto wake hao hapo mwezi wa Aprili mwaka huo. Mubarak anaendelea kubakia katika hospitali ya kijeshi kusini mwa kiunga cha Cairo juu ya kwamba hakuna sababu za kisheria za kuendelea kushikiliwa.

Watoto hao wa Mubarak walikuwa wamehukumiwa kifungo cha miaka minne gerezani kwa madai ya kutumia fedha za taifa kukarabati nyumba za familia. Baba yao alihukumiwa kifungo cha miaka mitatu katika kesi hiyo na baadae hukumu hizo zilikuja kutenguliwa mapema mwezi huu.

Maadhimisho ya miaka minne ya mapinduzi

Watoto wa Mubarak wanatoka gerezani ikiwa ni siku moja baada ya kutokea mapambano makali kati ya waandamanaji wanaopinga serikali na polisi kuadhimisha miaka minne ya kukomeshwa kwa utawala wake wa miaka 29.

Rais wa zamani wa Misri Hosni Mubarak(katikati) na watoto wake wakati wa kusikilizwa kwa mojawapo ya kesi zao mjini Cairo ,Gamal(kulia) na Alaa (kushoto).
Gamal Mubarak alitarajiwa kumrithi baba yake katika wadhifa wa urais.Picha: picture alliance/dpa

Ghasia hizo jana zimesababisha kuuwawa kwa watu 23,wakiwemo wanaume watatu ambapo serikali imesema wamekufa wakati wakitega mabomu na polisi watatu huku watu wengine 97 wakijeruhiwa.

Kati ya watoto hao wa Mubarak, Gamal alikuwa akionekana kama nguzo ya utawala wa mabavu na rushwa ambao kwa kushirikiana na matajiri wakubwa wa biashara wamekuwa wakifaidika kwa kuwanyonya wananchi maskini na wale waliokosa fursa nchini Misri.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AP/AFP

Mhariri : Iddi Ssessanga