1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watoto wa mitaani wasaka maisha Kenya

Lilian Mtono/ AFPE14 Aprili 2016

Nchini Kenya kunaongezeka na tatizo la watoto wa mitaani, ambao wanakataliwa na jamii hatua inayowasukuma kutafuta namna ya kuishi. Wakati hayo yanatokea, serikali haina mikakati madhubuti ya kukabiliana na tatizo hilo

https://p.dw.com/p/1IW3t
Strassenkinder in Afrika
Picha: picture-alliance/Ton Koene

Shirika la kimataifa linaloshughulika na ustawi na haki za watoto wa mitaani, CSC, inasema idadi ya watoto waishio mitaani nchini Kenya, inaweza kuwa kati ya 250,000 na 300,000, wakiwemo 60,000 ambao wako jijini Nairobi pekee.

Katika kitongoji cha Mlango Kubwa, katikati mwa jiji la Nairobi, sehemu lililopokuwa jalala hapo zamani ni kimbilio la watoto wa mitaani, ambapo wanapaita kama makao makuu. Kwa mujibu wa shirika hilo, katika eneo hilo watoto wanalala kwenye sakafu ngumu, karibu kabisa na eneo zinapotupwa takataka, ambako huokoteza mabaki ya takataka na kuyauza ili kupata fedha.

Watu huwaona watoto hawa kama si binadamu, anasema Moha, ambaye pia aliwahi kuwa mtoto wa mtaani, lakini hatimaye alifanikiwa kuyaacha maisha hayo magumu, na sasa ni mchezaji kwenye bendi za dansi. Anasema, watu wakiwaona wananusa gundi na wakiwa wachafu huwapiga na kuwatukana.

Baadhi yao hujiingiza kwenye maisha hayo baada ya kufiwa na wazazi wao, labda kutokana na ugonjwa wa Ukimwi na wengine hukimbia unyanyasaji majumbani kwao. Lakini wengine wanaishi mitaani kwa sababu tu familia zao zinaishi katika hali ya umaskini na haziwezi kuwalea. Moha anasema kuwa ni vigumu kuileezea hali wanayokumbana nayo, kwani unaweza kukuta kama wamelala nje ya duka la mtu, asubuhi mwenye duka badala ya kuwaamsha taratibu, huwapiga mateke au kuwamwagia maji.

Serikali inapaswa kuwasaidia

Wakiwa wametelekezwa na serikali, baadhi ya taasisi za kibinadamu huwasaidia. Alfajiri ni miongoni mwa taasisi hizo, na ni mradi uliobuniwa na msanii kutoka nchini Australia Lenore Boyd, anayewafundisha watoto hao sanaa ya uchoraji. "Kila mmoja anapaswa kufikiria namna watoto hawa wanavyochukuliwa, na ni kwa nini wanaishi mitaani na mateso wanayokutana nayo huko mitaani'', amesema Boyd. Watoto hawa wameathirika kimaisha, ni watoto waliopitia mateso makubwa, wametelekezwa. Kwenda mitaani ni hatua ya kukata tamaa.

Wasichana wanaosaidiwa
Wasichana wanaosaidiwaPicha: Leonie March

Wasichana ndio hukutana na wakati mgumu zaidi. Kituo cha kuwasaidia wasichana wanaoishi mitaani, The Rescue Dada, kilichopo Nairobi, kwa zaidi ya miongo miwili kimekuwa kikiwasaidia wasichana hao kwa kuwawezesha kurudi kwenye maisha yao ya kawaida. Kituo hicho kilicho na mabweni mawili na madarasa, kina wasichana 70 na kinatoa msaada wa kisaikolojia na elimu, na kuwezesha juhudi za kuwaunganisha tena na familia zao.

"Maisha ya mjini ni magumu sana. Mtu kulala nje, kwenye baridi na mara nyingine unanyeshewa mvua. Kuna wakati unaweza kuamka asubuhi na kukuta mwenzenu amekufa," anasema Janet, msichana mwenye umri wa miaka 16, aliyejiunga na kituo hicho hivi karibuni. Janet anasema wengine huishia kuuza miili yao ili kupata fedha za kununua chakula.

Miongoni mwa wasichana walioandikishwa kituoni hapo mwaka 2014, karibu theluthi yao walipitia unyanyasaji wa kingono, na wengine walibakwa na kundi la wanaume. Wengi wao walilazimishwa kuuza miili yao, huku kukiwa na hatari kubwa ya kupata Ukimwi.

Mkurugenzi wa kituo hicho Mary Njeri Gatitu, anasema kuwasaidia kurudi katika maisha yao ya kawaida kutachukua muda mrefu, ingawa anafanya kila linalowezekana kusaidia kile anachoamini anaweza kukifanya. Anasema ni sawa na tone la maji kudondokea katika bahari, kwa sababu serikali haijalishughulikia vya kutosha suala la umasikini nchini Kenya.