1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watoto wa Iraq taabani kutokana na vita

Josephat Nyiro Charo1 Agosti 2014

Tume ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kuisaidia Iraq, UNAMI, imesema Iraq sasa imegeuka kuwa mahala hatari kabisa duniani kuwa mtoto.

https://p.dw.com/p/1CnPI
Bildergalerie Kinder Spielplätze im Irak
Watoto wa Iraq wakicheza soka, lakini sasa mambo yamegeuka kutokana na vitaPicha: picture-alliance/dpa

Tume hiyo inasema imeorodhesha visa kadhaa vya hujuma dhidi ya watoto vilivyofanywa na kundi la Dola la Kiislamu la Syria na eneo la Shamu, ISIS, ikiwa ni pamoja na udhalilishaji wa ngono na ubakaji, mauaji, kupigwa na kulazimishwa kusajiliwa kama wapiganaji au wanajeshi. Huku machafuko yakiendelea nchini humo, watoto ndio wanaokabiliwa na mateso makubwa zaidi ikilinganishwa na watu wengine.

Hali nchini Iraq inatisha, amesema Tirana Hassan, Mtafiti mwandamizi wa shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch. "Familia, zikiwemo zile zenye watoto zimenasa kwenye uwanja wa mapambano na wanalipa gharama kubwa," amesema Hassan wakati alipozungumza na shirika la habari la IPS.

Huku ikikaribia kutimia miezi miwili tangu kuzuka machafuko nchini Iraq kati ya wanamgambo wa kiislamu na vikosi vya serikali, idadi ya raia waliouwawa imeongezeka. Tume ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kuisadia Iraq, UNAMI, imesema mnano mwezi Juni watu 1,500 waliuwawa, idadi inayoelezwa kuwa kubwa zaidi ndani ya mwezi mmoja, tangu mwaka 2008. Wanaharakati pia wameripoti mauaji ya watoto yaliyosababishwa na mashambulizi ya kutokea angani yaliyofanywa na vikosi vya serikali na wapiganaji wa kundi la Dola la Kiislamu la Iraq na eneo la Shamu, ISIS.

Watoto wahitaji msaada haraka

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa kufikia mwanzoni mwa mwezi Juni mwaka huu takriban Wairaq milioni 1.2 walikuwa wameyakimbia makazi yao kwa sababu ya machafuko, wengi wao wakitafuta hifadhi katika makazi ya muda, kambi za wakimbizi wa ndani au kuishi na familia nyingine zilizowakaribisha. Alec Wargo, Afisa Mradi katika ofisi ya Mjumbe maalumu wa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya Watoto na Mizozo, amelimbia shirika la habari la IPS kwamba idadi kubwa ya watoto wa wakimbizi wa ndani wanahitaji msaada kwa haraka.

Irak Anschlag 24.07.2014
Basi lililoshambuliwa mjini Taji,kaskazini mwa BaghdadPicha: Reuters

Wargo aidha amesema kumekuwa na taarifa za watoto kusajiliwa na wapiganaji na makundi yaliyojihami na silaha na wanauwawa au kujeruhiwa kwenye mapigano. Afisa huyo amesema maafisa wa Umoja wa Mataifa na serikali ya Iraq wamekuwa wakishirikiana kukabiliana na hali hiyo. Mpaka sasa hakujatolewa ripoti rasmi kuhusu hali ya watoto katika maeneo yanayodhibitiwa na kundi la wanamgambo la Dola la Kiislamu la Iraq, lakini Wargo amesema hali si nzuri kabisa.

Katika maeneo yanayodhibitiwa na serikali Umoja wa Mataifa umesema una wasiwasi mkubwa kuhusu hatua ya serikali kuzembea na kutochukua hatua zozote madhubuti kukabiliana na athari za mzozo unaoendelea kwa watoto.

Mateso dhidi ya watoto hayaripoti vizuri

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, mateso dhidi ya watoto nchini Iraq huenda hayaripotiwi ipasavyo, hasa kuhusu utekaji nyara, kutokana na changamoto za ukusanyaji taarifa na familia kusita kuripoti visa hivyo kwa polisi. Hakuna takwimu rasmi kuhusu idadi ya watoto waliosajiliwa kama wanajeshi, lakini Tume ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kuisaidia Iraq, UNAMI, imesema imepokea taarifa kuhusu watoto kusajiliwa na pande zote zinazohasimana, vikiwemo vikosi vinavyoegemea upande wa serikali.

Tume hiyo imesema watoto wametumiwa kama wapashaji habari, na katika badhi ya visa kama washambuliaji wa kujilipua kwa mabomu, kusimamia vituo vya upekuzi na kupigana vitani.

Bagdad Straße Anschlag 26.96.2014
Shambulizi katika barabara ya mji mkuu BaghdadPicha: Reuters

Richard Clarke, Mkurugenzi wa shirika la kimataifa linalopambana na usajili wa watoto jeshini, Child Soldiers International, ameliambia shirika la habari la IPS ingawa serikali ya Iraq haina udhibiti wa maeneo kadhaa ya nchi, ina jukumu muhimu la msingi kuziheshimu na kuzilinda haki za watoto, na kuzuia usajili wao usio halali na kutumiwa katika shughuli za kijeshi.

Shirika hilo lenye makao yake makuu mjini London, Uingereza linafanya kazi kuzuia usajili wa watoto jeshini na kuwasaidia kurejea katika maisha ya kawaida katika jamii wanapotoka uwanja wa vita. Clarke pia amesema serikali ya Iraq lazima uchukue hatua zote zinazostahiki kisheria na kisera kukomesha kabisa na kuepusha usajili wa watoto na vikosi vilivyo chini ya mamlaka yake na inapaswa iombe msaada wa mashirika ya kimataifa kuifikia azma hii.

Mwandishi: Josephat Charo /IPS

Mhariri: Mohammed Khelef