1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watoto ndiyo waathiriwa wakubwa wa mzozo wa Syria

29 Novemba 2013

Umoja wa Mataifa umeonya kuwa watoto wa Syria ndiyo waathiriwa wakubwa wa vita ambavyo vinaendelea nchini humo kwa zaidi ya miezi thelathini sasa huku wengi sasa wakilazimika kuwa wakimbizi na kuathirika kiakili.

https://p.dw.com/p/1AQRR
Picha: Reuters

Kulingana na shirika la umoja wa Mataifa linaloshughulikia maslahi ya watoto UNICEF, takriban watoto milioni 1.5 wa Syria wamelazimika kutoroka makwao na kukimbilia usalama katika nchi jirani.

Mkuu wa idara ya ulinzi wa kimataifa wa watoto wa UNHCR, Volker Tuks, amesema ulimwengu hauna budi bali kukumbushwa hili kuwa huku mzozo ukiendelea Syria, mamilioni ya watoto wanahangaika na kutaabika pakubwa.

Turks amesema katika kipindi cha miaka 20 iliyopita, tangu kutokea kwa mauaji ya halaiki ya Rwanda, hakuna mzozo mwingine umefikia kiwango cha Syria na kwamba watoto hao wanaathirika kisaikolojia kutokana na kuona umwagaji mkubwa wa damu na ugumu wa maisha.

Watoto wameathirika kisaikolojia

Kiasi ya watoto wengine milioni tatu wamesalia ndani ya Syria kama waathiriwa wa vita. Katika ripoti hiyo ya kurasa 60 iliyochapishwa hapo jana iliyopewa jina 'Damu ya Wasyria imefurika hadi magotini mwa wanadamu', watoto wanaelezea wanayopitia kupitia michoro na kuzungumzia uovu waliouona.

Watoto wa Syria wakisubiri kupokea huduma za matibabu
Watoto wa Syria wakisubiri kupokea huduma za matibabuPicha: picture-alliance/dpa/Vassil Donev

Baadhi ya watoto hao wanachora michoro inayoonyesha matumizi ya silaha na miili ya watu waliokufa huku wakipoteza matumaini ya kuwa na sehemu watakayoiita nyumbani kulikojaa amani, upendo na usalama.

Wengi wa watoto waliohojiwa wanaonyesha dalili za kusumbuka kimawazo kwa kukosa usingizi, kuwa wanyamavu kupita kiasi, kuwa na kigugumizi na kukojoa vitandani hali ambazo hawakuwa nazo kabla ya vita. Watoto wengi wa kiume wanaonyesha hasira na wanataka kurudi Syria kupigana.

Mbali na matatizo ya kisaikolojia wengine wamepata majeraha ya mwili. Kiasi ya watoto 741 wa Syria walitibiwa nchini Lebanon katika kipindi cha miezi sita ya kwanza ya mwaka huu huku wengine 1,000 wakipokea huduma za matibabu katika kambi ya wakimbizi ya Zaatari nchini Jordan.

Ongezeko la wakimbizi katika nchi jirani zimezua tatizo la kuwepo uhaba wa chakula, maji huduma za matibabu na makaazi na hata pia kusababisha msongamano mkubwa katika mfumo wao wa elimu.

Mahitaji ya kimsingi ukimbizini ni haba

Kwa mfano nchini Lebanon, idadi ya watoto wa Syria katika shule za umma inalingana na ya wa Lebanon ambayo ni watoto laki tatu huku watoto wengine laki saba wa Lebanon wakiwa katika shule za kibinafsi.

Watoto wa Syria wakisafirisha mali yao katika kambi nchini Jordan
Watoto wa Syria wakisafirisha mali yao katika kambi nchini JordanPicha: Getty Images

Ni nusu ya watoto walio Lebanon wa kutoka Syria wanaopata elimu ya msingi. Zaidi ya hayo pia wanalazimika kufanya ajira ili kuzisaidia familia zao. Wengi wa watoto hawa wakimbizi wanaishi katika mfumo wa familia zilizosambaratika.

Zaidi ya familia 70,000 zinaishi bila baba na zaidi ya watoto 3,700 wanaishi pekee yao bila jamaa zao au bila ya wazazi wao kama wakimbizi.

Umoja wa Mataifa umeitaka jumuiya ya kimataifa kutoa misaada ya kuwasaidia zaidi ya wakimbizi milioni tatu wanaohitaji misaada ya dharura.

Zaidi ya watu laki moja wameuawa katika vita hivyo vya wenyewe kwa wenyewe tangu vilipoanza mwezi Machi mwaka 2011 kutaka kumng'oa madarakani Rais Bashar al Assad.

Huku raia wa Syria wakiendelea kuhangaika na kuishi maisha ya dhiki wanajeshi wa Assad na waasi wanaendeleza mapigano ndani ya Syria na mkutano wa kimataifa wa kutafuta amani Syria ukipangiwa kufanyika mwezi Januari huku kukiwa na mashaka mengi kuhusu maandalizi yake.

Mwandishi: Caro Robi/afp/dpa

Mhariri: Josephat Charo