1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watoto bado wafanyishwa kazi za sulubu

12 Juni 2007

Watoto wanafanyishwa kazi katika kila pembe ya dunia, naiwe wale wanaochimba mawe nchini Peru, wanapaka ngozi rangi nchini Misri au wanaosuka mazuliwa nchini Pakistan. Wataalam wa shirika la ajira la kimataifa ILO mjini Geneva wanakadiria kuna watoto 250 milioni wanaofanyishwa kazi kote ulimwenguni na hasa katika nchi zinazoinukia. Wengi wao wanafanya kazi za hatari kwa maisha yao kwasababu hawana elimu, hawana maarifa au kwasababu vyombo vya kufanyia kazi wanavyopewa mara nyingi ni vyombo vya watuwazima.

https://p.dw.com/p/CB3g
Picha: AP

Kuna aina nyengine pia ya kazi za watoto - nayo ni ile ya watoto kulazimishwa kwenda kuomba, kuuza miili yao au kuiba majiani. Katika kila aina ya kazi za watoto, kuna watuwazima nyuma yake, wanaojitajirisha kwa nguvu za watoto, anasema Karl Zawadzky katika uchambuzi wake:

Kuwafanyisha kazi watoto ni aibu kwasababu jamii hiyo dhaifu miongoni mwa jamii sio tuu wanadhulumiwa, hawalipwi mishahara inayostahiki,bali pia wananyimwa utoto wao.Wanafanyakazi mtindo mmoja kama watu wazima.Wanakandamizwa na kuishi katika hali duni inayodhuru afya yao,miili yao na kudhoofisha akili yao pia.Watoto wanatengwa na wazee wao-wanafanyishwa kazi kama watumwa.Hawana hata matumaini ya maisha bora ya siku za mbele-kinyume kabisa,wengi wao wanakabiliwa na kitisho cha kuiaga dunia hata kabla ya wakati.

Miito na nasaha hazisaidii kitu kuling’owa balaa hilo.Cha maana ni kuzitafuta na kuzijua sababu za kiuchumi na kijamii za hali hiyo na kuzipatia ufumbuzi.

Kwasababu kazi ya watoto si matokeo ya dhamiri mbaya,bali ni matokeo ya mzozo wa kiuchumi katika nchi zinazoinukia pamoja pia na mashindano ya kibiashara kati ya nchi hizo na zile zilizoendelea kiviwanda.

Kusema kweli kuwadhulumu watoto chanzo chake ni umasikini.Takriban katika nchi zote za dunia mitindo ya kuwafanyisha kazi watoto imepigwa marufuku.Lakini bado shughuli hizo haramu zinaendelezwa kama njia ya kupunguza ukosefu ajira na kuimarisha mashindano ya kibiashara.Ni muhimu kwa hivyo kila wakati kuwatahadharisha walimwengu juu ya maafa yanayotokana na mitindo ya kuwanyanyasa watoto.Hakuna njia nyengine kwasababu hata taarifa na maazimio hayasaidii kitu kuzuwia watoto wasifanyishwe kazi.

Mazimio yako, tena ya kutosha,mfano lile lililofikiwa na hadhara kuu ya Umoja wa mataifa mwaka 1959 ,lijulikanalo kama “Azimio la haki za watoto.”

Katika azimio hilo imetajwa wazi kabisa kwamba watoto kabla ya kufikia umri maalum hawaruhisiwi kufanya kazi ambayo itadhuhru afya yao,masomo yao na itakayokorofisha hali yao ya kujiendeleza.Makubaliano ya shirika la kazi la kimataifa yanazungumzia juu ya umri wa miaka kumi kua ndio umri nwa chini ambao mtoto anaweza kufanya kazi ndogo ndogo na nyepesi.Kutiwa kazini watoto wadogo kuliko hao ni marufuku kabisa.

Dhahiri pia ni kwamba kazi ya watoto isiangaliwe pekee kwa jicho la nchi tajiri za viwanda zilizojiepusha na balaa hilo tangu miongo kadhaa iliyopita. Kuna nchi zinazoinukia ambako mtoto mwenye umri wa miaka 16 anaangaliwa kua ni mtu mzima,wakati mwengine anakua ameshaowa au kuolewa na kuzaa pia.

Katika nchi nyingi za ulimwengu watatu ukosefu ajira uliokithiri huangaliwa kua ni jambo la kawaida.Katika nchi kama hizo hakuna bima ya ukosefu ajira au ruzuku nyengine kutoka serikalini.Katika hali kama hii ,na katika familia nyingi kazi ya watoto ndio njia pekee muhimu ya kujipatia pato ziada-na mara nyingi kazi ya watoto ndio njia pekee ya kuhui maisha ya familia nzima.Lakini ajira ya watoto inaifanya iongezeke idadi ya watu wazima wasiokua na kazi .Inazidisha pengo lililoko kati ya wanaojimudu kifedha na wasiojiweza.Kwakua ajira ya watzoto ni matokeo ya umaskini,tatizo hilo haliwezi kutatuliwa vivi hivi tuu.Panahitajika mbinu madhubuti za kuinua elimu na mafunzo ya kazi.Watoto hawastahiki kufanyishwa kazi,wanabidi wende shule.