Watoto 80 waliokamatwa Chad waachiliwa huru
9 Desemba 2022Mwendessha mashtaka mkuu wa Chad, Wade Djibrine, amesema ombi la kutaka watoto hao waachiliwe huru liliwasilishwa na jaji akalikubali, lakini bado mashtaka dhidi ya watoto hao yanaendelea.
Mamia ya watu walikamatwa na kushikiliwa na maafisa wa usalama kufuatia maandamano ya vurugu dhidi ya utawala wa kijeshi wa Chad mnamo mwezi Oktoba. Miongoni mwa waliokamatwa, 262 tayari wamehukumiwa kifungo cha hadi miaka mitatu jela.
Maandamano hayo ambayo hayakuruhusiwa na serikali yalifanyika tarehe 20 Oktoba, kulikumbusha jeshi tarehe ambayo awali liliahidi kuacha madaraka ili kuruhusu utawala wa kidemokrasia.
Soma pia. Chad: mwaka mmoja baada ya kifo cha Déby
Hata hivyo, jeshi halikutimiza ahadi hiyo na badala yake, tarehe ya kuachia madaraka ilirefushwa kwa miaka miwili zaidi.
Kulingana na takwimu rasmi za serikali, watu 50 waliuawa kwenye maandamano hayo ya vurugu wakiwemo maafisa 10 wa usalama.
Lakini makundi ya upinzani yanasema idadi kamili ya waliouawa ni juu kuliko takwimu inayotolewa na serikali. Makundi hayo yamedai kwamba raia ambao hawakuwa na silaha waliuawa bila hatia.
Mtawala wa kijeshi wa Chad, Jenerali Mahat Idriss Deby Into, aliwashutumu waandamanaji kwa kile alichokitaja kuwa uasi na kujaribu kufanya mapinduzi.
Soma pia: Chad yataja serikali mpya ya mpito
Maafisa wamesema watu 601 wakiwemo watoto 83 walitiwa mbaroni katika mji mkuu, N'Djamena, pekee na kupelekwa katika gereza lenye ulinzi mkali la Koro Toro lililoko jangwani umbali wa kilomita 600 kutoka mji mkuu huo.
Jumla ya watu 401 walifunguliwa mashtaka katika mahakama iliyoko gerezani, na mawakili waliopinga jinsi kesi hizo zinashughulikiwa walisusia kuhudhuria vikao vya kortini vya kusikiliza kesi hizo.
Baada ya siku nne ya kesi kusikilizwa mahakamani, washukiwa 262 walikutikana na hatia na walihukumiwa vifungo vya kati ya miaka miwili na miaka mitatu.
Mwendesha mashtaka amesema washukiwa wengine 80 waliachiliwa kwa masharti, na washukiwa 59 waliachiliwa huru.
Deby mwenye umri wa miaka 38 alichukua madaraka baada ya baba yake, Idriss Deby Itno, kuuawa kwenye operesheni dhidi ya waasi mwezi Aprili 2021.
Kabla ya kuuawa kwake, marehemu Idriss Deby alikuwa ameliongoza taifa hilo la Sahel kwa miaka 30.
(AFPE)
Tafsiri: John Juma
Mhariri: Mohammed Khelef