Watetezi haki za binaadamu Tanzania watishwa
3 Aprili 2019Ripoti hiyo ya kurasa 120 iliyozinduliwa Jumatano (Aprili 3) ikijumuisha pia kundi la waandishi wa habari na iliyokusanya taarifa kutoka mikoa mbalimbali kupitia watetezi na wawakilishi wa mtandao huo pamoja na Baraza la Habari Tanzania (MCT), inaonesha kiwango cha matukio ya ukiukwaji wa watetezi wa haki za binadamu kinaongezeka huku wakuu wa wilaya, mikoa na jeshi la polisi wakiwa ndio wahusika wakuu wa matendo hayo.
Ripoti hiyo inayoangazia mwaka 2018 pekee inaonesha matukio zaidi ya 50 yaliyoripotiwa kukiuka haki za watetezi wa haki za binaadamu, yakiwemo ya kukashifiwa hadharani, kubandikwa majina ya udhalilishaji, kutekwa, kubambikiziwa kesi ambazo wanapofika mahakamani huonekana hawana hatia, na pia kuzigeuza shughuli halali za uandishi wa habari kuwa uhalifu.
Onesmo ole Ngurumo, mratibu wa mtandao huo, aliwaambia wanahabari kwamba kuanzia kipindi cha mwaka 2013 walipoanza kutoa ripoti hiyo, "hali inazidi kuwa mbaya kwa kundi hilo linalojizatiti kuhakikisha nchi inatekeleza na kustawisha haki za binaadamu kama inavyozingatiwa na katiba na nchi kuridhia mikataba mbalimbali ya kimataifa."
Mkasa wa Loliondo
Miongoni mwa matukio yanayoelezewa kwenye ripoti hiyo, ni lile la watetezi waliopo katika eneo la Loliondo kaskazini mwa Tanzania, ambao wanakumbana na mazingira magumu zaidi. Ripoti inatoa wito wa "uingiliaji kati wa haraka kutokana na watetezi hao kuwa katikati ya mgogoro baina ya wakaazi na muwekezaji," ambapo wananchi wa eneo hilo walihamishwa kwa nguvu huku jeshi la polisi likisimamia zoezi hilo lililowacha idadi kubwa ya watu bila makaazi na uharibifu mkubwa wa mali.
Deogratias Bwire, wakili kutoka katika mtandao huo aliiambia DW kuwa baadhi ya watetezi wa haki za binadamu wa eneo hilo walikamatwa na wengine kufunguliwa mashitaka na kesi zinaendelea.
Aidha, watetezi hao wa haki za binaadamu waliweka wazi kwamba uhuru wa kujieleza kupitia vyombo vya habari umevamiwa, kiasi cha kwamba sasa si rahisi tena wao kuzungumza na wananchi kupitia vyombo hivyo rasmi, kwani vinatozwa faini kubwa na hivyo kukosa wasaa wa kuongea na wananchi.
Kuzinduliwa kwa ripoti hiyo kunaenda sambamba na kuzinduliwa kwa bango kitita la sheria na sera zinazoathiri nafasi ya asasi za kuraia nchini Tanzania, ambapo sheria mbalimbali zimeonekana kudhoofisha shughuli za watetezi hao, ikiwemo Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari na Sheria ya Takwimu.
Habari hii imeandikwa na Hawa Bihoga, DW Dar es Salaam