1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watanzania washiriki uchaguzi wa serikali za mitaa

28 Novemba 2024

Watanzania wametekeleza jukumu lao la kikatiba kwa kuchagua viongozi wa serikali za mitaa huku mauaji ya makada wa chama kikuu cha upinzani Chadema yakitia dosari zoezi hilo lililofanyika nchi nzima.

https://p.dw.com/p/4nUkO
Tansania Kommunalwahlen 2024
Baadhi ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam wakiwa katika foleni ya kupiga kura katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa.Picha: Eric Amos/DW

Zoezi la upigaji wa kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa hapa nchini limefungwa leo saa 10 jioni huku kukiwa na taarifa za mauaji ya makada wa Chadema, ambao baadhi walikuwa ni wagombea katika uchaguzi huu. Chadema walitoa taarifa kupitia mtandao wa X, na kueleza kuwa makada wawili wa chama hicho, akiwamo George Mgombea wa nafasi ya uenyekiti wa Kitongoji, cha Stand, kata ya Mkwese, Jimbo la Manyoni, aliuawa kwa risasi akiwa nyumbani kwake.

Kadhalika, kada mwingine Steven Chalamila, mkazi wa  Tunduma ameuawa baada ya kukatwakatwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake. Kadhalika mgombea nafasi ya ujumbe kata ya Gongolamboto, Modestus Timbilisimwa, naye anadaiwa kuuawa.

Ufafanuzi wa jeshi la polisi kuhusu kifo cha kada wa Chadema

Tansania Kommunalwahlen 2024
Polisi wakikabiliana na mtu walietofautiana nae katika mchakato wa uchaguzi jijini Dar es SalaamPicha: Eric Amos/DW

Akifafanua tukio la kuuawa kwa George Mohamed Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Singida (SACP), Amon Kakwele amesema "Hivyo kupelekea kufyatua risasi hewani ili kuwatawanya watu hao lakini kwa bahati mbaya risasi hiyo ilimjeruhi mtu mmoja, George Juma mwenye umri wa miaka 41, ambaye alikuwa ni mgombe wa nafasi ya uenyekiti wa kitongoji”

Kadhalika Chadema wamedai kukamata karatasi za kupigia kura ambazo tayari zimeshapigwa katika baadhi ya maeneo nchini. Wakati hayo yakijiri, zoezi la upigaji kura katika maeneo mengine limeendelea vizuri ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, alipiga kura jijini Dodoma na akiwa huko amesisitiza kulinda amani."Wakapige kura kwa maelewano na masanduku yanavyosema ndo hivyo matokeo yatoke."

Tansania Kommunalwahlen 2024
Baadhi ya wapiga kura wakiwa chini ya ulinzi wa polisi jijini Dar es SalaamPicha: Eric Amos/DW

Kwa upande wake, Waziri anayesimamia Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(tamiSEMI) Mohamed Mchengerwa amesema anatarajia matokeo kutangazwa ndani ya saa 72. "Kwa mifumo tuliyonayo sasa tunaamini kwamba zoezi hili litakuwa la muda mfupi tu, yako maeneo leo watafahamu walioshida na baadhi yao maeneo kesho watafahamu walioshinda"

Changamoto ya kuhakiki majina ya wapiga kura

Katika hatua nyingine baadhi ya Watanzania walioshiriki zoezi hilo wamesema kumekuwa na changamoto kadhaa katika kuhakiki majina yao kabla ya kupiga kura. Celestina Mushi, mkazi wa  Sinza, amesema "Kwa hiyo mtu atafute herufi zimechanganywa, mpaka aje apate wengine wamehangaika mpaka muda umeisha wamerudi wamerudi bila kupiga kura, wengine wamechoka, wamerudi bila kupiga kura.

Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unafanyika kila baada ya miaka mitano na kuwapa wananchi nafasi ya kuchagua wenyeviti wa vijiji, mitaa, vitongoji na wajumbe wa halmashauri.

DW: Dar es Salaam