1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wagombea watatu wanaoongoza kuelekea uchaguzi DRC

Yusra Buwayhid
29 Desemba 2018

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ikiwa inaelekea katika uchaguzi mkuu Desemba 30, wagombea watatu ndiyo wanaoonekana kuongoza mstari wa mbele kati ya idadi jumla ya wagombea 21 wanaowania urais katika taifa hilo.

https://p.dw.com/p/3AkqG
23.04.2014 Karte Congo DRC train crash Katanga map

Mmoja wao ni, Emmanuel Ramazani Shadary, 58, na ambaye anatajwa kuwa ni kibaraka wa rais Joseph Kabila.

"Iwapo Shadary atashinda uchaguzi wa Jumapili basi Kabila ataendelea kuiongoza nchi chini kwa chini," anasema Indigo Ellis kutoka kampuni ya Verisk Maplecroft inayotoa ushauri wa kimkakati wa masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.

"Shadary hana sifa zozote za maana zaidi ya kuwa mtiifu kwa Kabila", mchambuzi wa shirika la kisiasa lisilo la kiserikali la mjini Kinshasa aliyekataa kutajwa kwa jina ameliambia shirika la habari la AFP.

Shadary alikuwa waziri wa mambo ya ndani wakati wa kipindi cha machafuko ya waandamanaji mwishoni mwa 2016, baada ya Kabila kung'ang'ania madaraka kinyume na katiba.

Kongo Emmanuel Ramazani Shadary
Emmanuel Ramazani Shadary, mgombea urais chama tawala DRCPicha: REUTERS

Shadary na maafisa wengine 13 wa serikali wanakabiliana na vikwazo vya Umoja wa Ulaya kwa madai ya kukiuka haki za binadamu. Kwa kulipiza kisasi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo iliutaka Umoja wa Ulaya kuondoa ujumbe wake katika mji mkuu wa Kinshasa ifikapo siku ya uchaguzi.

Shadary mwanzoni aliingia katika uwanja wa siasa kama mwanachama wa UDPS, chama cha upinzani kikongwe na kikubwa zaidi nchini humo. Mwaka 1997, baada ya kuondolewa madarakani dikteta Mobutu Sese Seko, Shadary alichaguliwa kama makamu wa gavana wa mkoa wa Maniema na mwaka mmoja baadaye akawa gavana.

Baada ya Kabila kuchukua mamlaka mwaka 2001 kufuatia mauaji ya baba yake, Shadary alimsaidia mwaka mmoja baadaye kuunda chama cha People's Party for Reconstruction and Democracy (PPRD). Na sasa Shadary ndiye katibu wa kudumu wa chama hicho.

Shadary anazungumza Kiswahili na Lingala, lugha mbili zinazotumika zaidi mashariki na magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Shadary ni Mkatoliki, na ana watoto wanane.

Tshisekedi, mgombea mwenye diplomasia

Mgombea wa pili ni Felix Tshisekedi, 55, ambaye anatarajia kushinda uchaguzi huo na kuweza hatimaye kuwa rais wa taifa hilo jambo lilomshinda baba yake Etienne, aliyeanzisha chama kikuu cha upinzani nchini humo, the Union for Democracy and Social Progress (UDPS), mnamo 1982. Tshisekedi mtoto alichukua hatamu ya uongozi wa chama hicho baada ya baba yake kufariki dunia Febuari 2017.

Anajulikana miongoni mwa marafiki zake kwa jina la utani la "Fatshi" na alipata diploma katika masomo ya masoko na mawasiliano nchini Ubelgiji. Lakini hakuwahi kuwa na wadhifa wa ngazi ya juu, hana uzoefu wa usimamizi na amekosa haiba aliyokuwa nayo baba yake.

DR Kongo Felix Tshisekedi
Felix Tshisekedi mgombea urais upande wa upinzani chama cha UDPSPicha: Getty Images/AFP/N. Maeterlinck

"Etienne alikuwa mkaidi na mwenye kiburi," anasema mwangalizi mmoja wa upande wa upinzani nchini humo. (Lakini) Felix ni mtu mwenye diplomasia, na yupo tayari zaidi kusikiliza maoni ya wengine."

Mnamo Novemba 11, Tshisekedi aliungana na viongozi wengie sita wa upinzani na kutaka kusimamisha mgombea mmoja, Martin Fayulu, ili apambane na Shadary. Lakini mpango huo ulishindikana na kukataliwa na vigogo wa chama chake. Tshisekedi na kiongozi mwengine wa upinzani Vital Kamerhe polepole walijivuta kutoka katika mpango huo, hatua iloudhoofisha na kuugawa upinzani nchini humo. Ni baba mwenye watoto watano na anahudhuria kanisa la Pentecostal sawa na Fayulu mjini Kinshasa.

Fayulu, mkosoaji mkubwa wa Kabila

Na Martin Fayulu,62, ni mgombea watatu katika wale walio mstari wa mbele. Hakuwa mwanasiasa anaejulikana kabla ya kusogea katika ngazi ya juu na kupata umaarufu wiki chache kabla ya uchaguzi. Fayulu ameanza kujulikana miaka miwili iliyopita kama mkosoaji mkubwa wa Kabila na kung'ang'ania kwake kubakia madarakani.

DR Kongo Wahlkampf Martin Fayulu
Martin Fayulu, mgombea urais upande wa upinzaniPicha: Reuters/S. Mambo

Mara nyingi huwa mstari wa mbele katika maandamano ya upinzani, ameshakamatwa mara kadhaa na hata kufyatuliwa risasi ya mpira kichwani. Ingawa chama chake cha  Engagement for Citizenship and Development kina viti vitatu tu bungeni, Fayulu alijulikana zaidi mwezi uliopita kufuatia kutangazwa mgombea wa muungano wa upinzani katika mkutano wao mjini Geneva. Lakini siku mbili baadaye makubaliano hayo ya viongozi wa upinzani yalisambaratika baada ya Felix Tshisekedi kujitoa aliposhinikizwa na chama chake, na badala yake aliamua kusimama kama mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho.

Fayulu amefanya kampeni kubwa na kutembelea maeneo mengi nchini humo kutangaza sera zake. Na pia kisiri siri anaungwa mkono na wanasiasa wawili magwiji - mbabe Jean-Pierre Bemba na mfanyabiashara Moise Katumbi, gavana wa zamani wa Katanga aliyeko uhamishoni. Wanasiasa hao wote wawili wamewekewa marufuku ya kushiriki katika uchaguzi wa Jumapili.

Kongo: Bildkombo Moise Katumbi und Jean-Pierre Bemba
Moise Katumbi (kushoto) na Jean-Pierre Bemba (kulia)

Fayulu amesoma nchini Ufaransa na Marekani, na baadaye 1984 kufanya kazi katika shirika la mafuta la Marekani linalojulikana kama Exxon Mobil. Alibaki katika kampuni hiyo kwa miongo miwili na kufanya kazi barani Afrika na baadaye kupandishwa cheo na kuwa mkurugenzi mkuu.

Iwapo atachaguliwa katika uchaguzi wa Jumapili, ameahidi kuwekeza dola bilioni 126 katika uchumi wa taifa hilo na kutengeneza nafasi za ajira milioni 20 katika kipindi cha miaka mitano ijayo. Anazungumza Lingala na anamiliki hoteli mjini Kinshasa ambayo iko karibu na nyumba ya Kabila pamoja na ofisi ya rais.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/afp

Mhariri: Sylvia Mwehozi