Wataliban waitikisa tena Pakistan
22 Novemba 2012Afisa kutoka ofisi ya mkuu wa wa mji wa Islamabad, Muhammad Haroon amesema mshambuliajo moja aliyevalia vesti yenye miripuko, aliushambulia msururu wa watu waliyokuwa wanafanya maandamano ya kidini mjini Rawalpindi, karibu na Islamabad kabla ya saa sita usiku wa kuamkia leo, na msemaji wa kikosi cha uokozi cha huduma ya 1122, Deeba Shehnazi, aliliambia shirika la habari la Ujerumani dpa, kuwa raia 23 waliuawa na wengine 62 kujeruhiwa, wakiwemo watoto nane na maafisa wanne wa polisi.
Mashambulizi yote yawalenga washia
Haroon alisema mripuaji anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 18 alijaribu kujipenyeza katika maandamano ya sherehe Muharram na baada ya kuzuiwa na wasimamizi waliyokuwa mlangoni, alijiripua. Aliongeza kuwa wamepata kichwa cha mripuaji huyo na wanafanya uchunguzi kuweza kumbaini. Watu wengine wawili waliuawa siku ya Jumatano katika matukio mengine mawili ya mabomu katika mji wa kusini wa Karachi. Kamishna wa polisi mjini Karachi, Hashim Raza, aliiambia dpa kuwa mashambulio yote yaliwalenga washia.
Pikipiki iliyopakizwa miripuko pia iliripuriwa karibu na mskiti wa washia mjini Orangi, na kuua mtu moja na kujeruhi wengine saba. Na katika tukio lingine bomu liliwekwa katika ukuta wa msikiti katika eneo hilo na kuua mtu mmoja na kujeruhi wengine wanane. Wanamgambo wa Taliban walidai kuhusika na mashambulizi yote matatu na kukiri kuwa yote yalikuwa yanalenga mikusanyiko ya waumini wa Shia. Msemaji wa kundi nchini Pakistan Ehsanullah Ehsan amesema washia walishambuliwa kwa sababu wanamkejeli mtume Muhammad na kitabu kitakatifu cha Qur-an.
Taliban wasema wataendelea na mashambulizi
Katika taarifa yake, Ehsan alisema wataendelea na mashambulizi bila kujali hatua za usalama zinazochukuliwa na waziri wa mambo ya ndani Rehman Malik. Waumini wa madhehebu ya Shia wanachangia asilimia 20 ya raia wa Pakistan. Mara nyingi washia huchukuliwa kama waasi na waumini wa madhehebu ya sunni ambao ndiyo wengi zaidi nchini humo, na wamekuwa wakishambuliwa na makundi ya waumini wenye misimamo mikali ya dini. Serikali imeimarisha ulinzi mahali ambapo washia wanakutana kuhudhuria sherehe ya Muharram ambapo wanaomboleza kifo cha Imam Hussein, ambaye ni mjukuu wa Mtume Muhammad.
Wakati huo huo rais Muhammad Mursi wa Misri ameahirisha kwenda Pakistan kuhudhuria mkutano huo ili kusimamia utekelezaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Hamas mjini Gaza, na badala yake amemtuma makamu wake Mahmoud Mekki. Nchi zinazohudhuria mkutano wa mjini Islamabad unaofahamika kama D8 ni pamoja na Bangladesh, Misri, Indonesia na Iran. Nyingine ni Malaysia, Nigeria, Pakistan na Uturuki.
Mwandishi: Iddi ISmail Ssessanga/dpae
Mhariri:Mohammed Abdul Rahman