1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wataalamu wa silaha za sumu kuanza kazi Syria

Admin.WagnerD2 Oktoba 2013

Wataalamu wa kimataifa wa kuharibu silaha za sumu wanatarajiwa kuanza shughuli ya kuziorodhesha silaha za sumu za Syria kwa kupitia orodha ya maeneo mbalimbali iliyotolewa na serikali ya Syria

https://p.dw.com/p/19sg8
Picha: STR/AFP/Getty Images

Kundi la wataalamu 19 wa shirika la kudhibiti silaha za sumu lenye makao yake The Hague OPCW liliwasili Damascus hapo jana kutekeleza azimio nambari 2118 lililopitishwa na baraza la usalama la umoja wa Mataifa linalotaka silaha hizo za Syria kuharibiwa ifikapo katikati ya mwaka ujao.

Kundi hilo linatarajiwa kuanza kazi yake siku moja tu baada ya upinzani nchini Syria kuonya kuwa kuna janga la kibinadaamu viungani mwa mji mkuu Damascus katika eneo la Moadamiyet al Sham mojawapo ya maeneo yanayoripotiwa kulengwa wakati wa shambulio la gesi ya sumu ya sarin tarehe 21 mwezi Agosti.

Pia inakuja baada ya waziri wa habari wa Syria kusisitiza kuwa rais Bashar al Assad atasalia madarakani na huenda akagombea kipindi kingine katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa mwaka ujao.

Je Assad ataondoka madarakani?

Kuondoka madarakani kwa Assad ni mojawapo ya matakwa ya upinzani Syria ambao unasisitiza kuondoka kwake ndiko kutakuwa msingi wa kuwepo kwa mkutano wa kimataifa wa kutafuta amani nchini humo unaotarajiwa kuandaliwa mjini Geneva.

Rais wa Syria Bashar al Assad
Rais wa Syria Bashar al AssadPicha: Reuters

Taarifa kutoka umoja wa Mataifa imesema wataalamu hao wa shirika la OPCW wanatarajiwa katika siku chache zijazo kuyahakiki na kuthibitisha maelezo yaliyotolewa na utawala wa Syria na kupnaga mipango ya mwanzo ya kuisadia Syria kuharibu silaha zake za sumu na kwamba wanatarajiwa kukamilisha zoezi hilo ifikapo tarehe moja mwezi ujao.

Ni kazi kubwa kuziharibu silaha za Syria

Wataalamu hao wana kibarua kikubwa kwani inaaminika kuwa syria ina zana za silaha hizo za tarkriban tani 1,000 ambazo zimehifadhiwa katika maeneo 45 kote nchini humo. Hii ndiyo mara ya kwanza kwa watalaamu wa shirika hilo la kudhibbiti silaha za sumu kuendesha shughuli zao ndani ya nchi inayokumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Wakati huo huo wataalamu wa umoja wa Mataifa waliokamilisha shughuli za uchunguzi wa silaha za sumu nchini Syria mapema wiki hii wanatarajiwa kutoa ripoti yao kamili na ya mwisho mwishoni mwa mwezi huu.

Katibu mkuu wa umoja wa Mataifa Ban ki Moon
Katibu mkuu wa umoja wa Mataifa Ban ki MoonPicha: picture alliance/abaca

Azimio hilo lililopitishwa na baraza la usalama la umoja wa Mataifa linataka pia kuwepo kwa mkutano wa amani mapema iwezekanavyo na katibu mkuu wa umoja wa Mataifa Ban ki Moon amesema amepanga kuuandaa katikati ya mwezi Novemba.

Hata hivyo uwezekano wa kuandaliwa kwa mkutano huo unatiliwa shaka kufuatia mvutano kati ya serikali ya Syria na upinzani.Muungano wa kitaifa wa upinzani Syria unaishutumu serikali kwa kuanzisha kampeini ya kutumia mbinu ya kuwanyima wakaazi wa Moadamiyet al Sham chakula.

Zaidi ya watu 115,000 wameuawa katika vita vya Syria na wengine milioni sita kulazimika kutoroka makwao.

Mwandishi:Caro Robi/afp/ap

Mhariri: Yusuf Saumu