Wasiwasi watanda nchini Kenya
1 Februari 2018Wanaharakati nchini Kenya wamekwenda mahakamani kuishtaki serikali ya nchi hiyo, kwa kuvifungia vituo vya televisheni kurusha matangazo tangu Jumanne. Na katika hali ya wasiwasi inayoendelea nchini humo, baadhi ya wanasiasa wa upinzani wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma za kuhusika na vitendo vya kuvuruga usalama wa taifa, akiwemo Mbunge wa Ruaraka T J Kajwang aliyesimamia shughuli yenye utata ya kumuapisha kinara wa upinzani Raila Odinga kuwa rais wa wananchi.
Mawakili wa mbunge wa Ruaraka T J Kajwang wa chama cha ODM, mojawapo ya vinavyounda muungano wa NASA wamefika katika mahakama ya milimani kutaka kujua mbivu na mbichi. Mbunge wa Ruaraka T J Kajwang alikamatwa na maafisa wa usalama jumatano jioni na kuzuiliwa usiku kucha katika kituo kimoja cha polisi eneo la Kiambu.Duru zinaeleza kuwa polisi wanaandaa mikakati ya kumshtaki kwa uhalifu mkubwa unaoadhibiwa kwa hukumu ya kifo. Nelson Havi ni mmoja wa mawakili wa Mbunge T J Kajwang na anaielezea hali halisi.
Kuna taarifa ambazo hazijathibitishwa, zinazodai kuwa serikali itamshitaki Kajwang kwa kufuata sharia za kipengee cha 59 na 60 ya uhalifu inayoangazia shughuli ya kula kiapo haramu.Kwa mujibu wa katiba yeyote anayeshiriki na kufanikisha mipango ya hafla ya kula kiapo haramu anaweza kuadhibiwa kwa hukumu ya kifo au kufungwa maisha.Mapema hii leo polisi wamerusha makopo ya gesi ya kutoa machozi kuwatawanya vijana waliokusanyika nje ya mahakama ya Milimani jijini Nairobi ambako kesi hii inasikilizwa.
Wakati huohuo mwanaharakati Okiya Omtatah amewasilisha kesi ya kuishtaki mamlaka ya mawasiliano na mawaziri wa Usalama wa Taifa Fred Matiangi na mwenzake wa mawasiliano ya teknoljia Joe Mucheru kwa kuidhinisha vituo vya televisheni kufungiwa kurusha matangazo na kusababisha hasara ya mamilioni ya fedha.Vituo vya televisheni vilifungwa tangu jumanne asubuhi ili kuwazuwia kurusha matangazo ya moja kwa moja ya hafla ya kumuapisha kiongozi wa upinzani wa NASA Raila Odinga kutokea bustani ya Uhuru. Baadhi ya wanahabari nao pia wanakabiliana na kitisho cha kukamatwa kwa tuhuma ya kuwasaidia wanasiasa wa upinzani kufanikisha shughuli hiyo.
Kwa upande mwengine wanasiasa wa upinzani wamemtolea rai Rais Uhuru Kenyatta kuwarejeshea ulinzi baadhi yao ambao walipokonywa walinzi.Kwenye barua yake, mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohamed aliweka bayana kuwa wanaolengwa ni wachache tu jambo ambalo linakiuka sharia na huenda likazua mitafaruku.Kwa mtazamo wao hatua hiyo inaashiria ubaguzi dhidi ya wanasiasa wa upinzani. Yoye hayo yakiendelea wanachama wa vuguvugu la NRM lililopigwa marufuku wanashikilia wako ngangari na kamwe hawatayumbishwa na chochote.Kwenye kikao na wandishi wa habari katika afisi za muungano wa NASA chini ya jukwaa la Okoa Kenya Miguna Miguna alisema wako imara zaidi.
Kwa sasa hatima ya muungano wa NASA haijaeleweka baada ya vinara wake wawili kususia hafla ya kumuapisha Raila Odinga siku ya Jumanne. Duru zinaeleza kuwa Raila Odinga yuko kwenye likizo fupi katika nchi jirani ya Tanzania.
Kutoka Nairobi mimi ni Thelma Mwadzaya
Mhariri: Daniel Gakuba.