1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wasiwasi Kenya baada ya 17 kuuawa, 60 kujeruhiwa

2 Julai 2012

Hali ya wasiwasi imetanda nchini Kenya kufuatia vifo vya watu 17 na wengine 60 kujeruhiwa mashambulizi mawili ya kigaidi yaliyotekelezwa katika makanisa mawili mjini Garissa hapo jana.

https://p.dw.com/p/15PWx
Maafisa wa usalama wa Kenya katika eneo la mashambulizi dhidi ya kanisa, Garissa.
Maafisa wa usalama wa Kenya katika eneo la mashambulizi dhidi ya kanisa, Garissa.Picha: Reuters

Ni tukio ambalo limezua hofu miongoni mwa raia kote nchini. Huku usalama ukiimarishwa katika sehemu za miji, maafisa zaidi wa usalama wamepelekwa mjini Garissa kuwasaka magaidi waliotekeleza mashambuliz hayo yaliyotekelezwa sambamba katika Kanisa la African Inland Church na Kanila Katoliki la Our Lady of Consolata.

Zaidi ya majeruhi 40 wanaendelea na matibabu katika hospitali kuu ya Garissa huku wengine waliopata majeraha mabaya wakipata matibabu katika hospitali kuu ya Kenyatta hapa Nairobi.

Maafisa wawili wa polisi waliokuwa wakishika doria katika kanisa la African Inland Church ni miongoni mwa waliouawa kwenye shambulizi hilo.

Jumla ya watu 17 wamethibitishwa kufariki kwenye mashambulizi hayo wakiwemo watoto watatu.

Wanajeshi wa Kenya wakilinda mpaka katika na nchi yao na Somalia.
Wanajeshi wa Kenya wakilinda mpaka katika na nchi yao na Somalia.Picha: AP

Shirika la Msalaba Mwekundu nchini Kenya limetoa mwito wa dharura wa mchango wa damu kuwasaidia majehuri wanaohitaji kufanyiwa upasuaji. Kufikia sasa Hakuna mshukiwa yeyote aliyekamatwa kuhusiana na mashambulizi ya hapo jana.

Serikali kupitia wizara ya usalama wa kitaifa inatarajiwa kutoa taarifa kamili juu ya mashambulizi hayo. Rais Mwai Kibaki ameagiza msako mkali kufanywa ili kuwata mbaroni magaidi hao.

Kenya imekumbwa na mashambulizi ya kigaidi kutoka kwa watu wanaoaminika kuwa wanachama wa kundi la al-Shabaab kutoka nchi jirani ya Somalia tangu majeshi ya Kenya yaingie ndani ya Somalia mwezi Oktoba mwaka uliopita kuwasaka wanachama wa kundi hilo waliohusika katika utekajinyara wa raia wa kigeni na wahudumu wa mashirika ya misaada.

Ripoti: Alfred Kiti/DW Nairobi
Mhariri: Mohammed Khelef