Wasifu wa Peer Steinbrück, mpinzani wa Merkel
10 Septemba 2013"Yeye anaweza." Kansela wa zamani wa Ujerumani, Helmut Schmidt, kutoka chama cha SPD tayari amelitamka hilo hapo mwaka 2011 kuhusu Peer Steinbrück, rafiki na mwanachama mwenzake na hajamsifu tu kwa sifa walizonazo kwa pamoja katika mchezo wa dama.
Kwa Schmdit lilikuwa sio jambo muhimu kwake kwamba Steinbrück kutoka Hamburg mwenye umri wa miaka 66 na mwenye shahada ya uchumi na aliewahi kuwa waziri wa fedha wa Ujerumani, alipata matokeo mabaya katika somo la hesabu wakati alipokuwa mwanafunzi na ilibidi arudie mara mbili ili kuweza kupata cheti cha kumaliza shule ya sekondari.
Muhimu kwa Schmidt kumpendekeza kulitokana zaidi na na maarifa ya masomo ya kiuchumi aliyokuwa nayo Steinbrück kutokana na kuwa Mshauri katika Ofisi ya Kansela kuanzia mwaka 1978 hadi mwaka 1981 chini ya utawala wa Helmut Schmidt kwa kupitia nyadhifa mbali mbali za serikali na wizara kuwa Waziri Mkuu wa jimbo la North Rhine - Westphalia na hadi hatimae kuwa wazirí wa fedha katika serikali Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani ambapo ameshika wadhifa huo hapo mwaka 2005.
Ilikuwa ni mara tu baada ya kushindwa na chama cha CDU katika uchaguzi wa jimbo la North Rhine-Westphalia akiwa mgombea mkuu wa chama cha SPD ambapo muda mfupi baada ya hapo aliyekuwa mgombea wa ukansela wakati huo, Angela Merkel, baada ya uchaguzi huo ilibidi kwa ushirikiano wa chama chake cha CDU na CSU waunde serikali ya muungano mkuu kwa kushirikiana na chama cha Social Demokratic.
Steinbrück kama waziri wa fedha wa Merkel
Chama ha SPD kilimpendekeza Peer Steinbrück kuwa waziri wa fedha katika serikali hiyo ya muugano mkuu. Katika wadhifa huo alishirikiana kwa karibu na kwa uaminifu na Merkel kupambana na mzozo wa fedha.
Wakati mzozo huo ulipopamba moto hapo mwaka 2009 watu waliokuwa wameweka akiba kwenye benki za Ujerumani walitishia kuondosha fedha kwenye benki hizo na kwa pamoja Steinbrück na Merkel walijitokeza hadharani na kuhakikisha fedha zote zilizowekwa kwenye mabenki ya Ujerumani zitakuwa salama.
Akiwa kama waziri wa fedha kabla ya kuzuka kwa mzozo wa fedha Steinbrück pia alipitisha taratibu nyingi za fedha zilizosusha utata.Kwa mfano kuendeleza wawekezaji wa majumba na utaratibu wao wa kukusanya mikopo ili kuja kuiuza baadae.
Udhaifu wa kisiasa wa Steinbrück
Mtindo wa kisiasa wa Steinbrück unaonekana kuwa wa kifidhuli, unaelimisha na sio wa kidiplomasia, kutokana na kwamba mara nyingi hutamka moja kwa moja kile anachofikiria. Wenzake pia wanamuelezea kuwa ni mtu asiekuwa na subira kabisa.
Linapokuja suala la kuzuwiya ukwepaji kodi alitishia kuchukuwa hatua ya mabavu na alikataa kubadilishana data na Uswisi iliokuwa inajulikana kama sehemu ya kuweka fedha za magendo. Rai yake ya kupambana na nchi hiyo ilisababisha mzozo mkubwa wa kidiplomasia.
Tokea wakati alipokuwa waziri wa fedha wa serikali ya Ujerumani na waziri mkuu wa jimbo la North Rhine -Westphalia Peer Steinbrück alikuwa akiunga mkono kile kilichokuwa kinajulikana kama "Agenda 2010".
Gerhard Schroeder, kansela wa zamani kutokea pia chama cha SPD, katika mpango wake huo wa mageuzi makubwa, alitaka kulijenga upya soko la ajira na baadae kupunguza ukosefu mkubwa wa ajira.
Mpango huo ulijumuisha juhudi za kupunguza msaada wa huduma za serikali na kutaka watu wawajibike zaidi katika kipindi hicho cha ukosefu wa ajira, kurahisisha mazingira ya kazi za kondarasi na kusaidiwa na kundelezwa kwa sekta ya mishahara ya kiwango cha chini.
Steinbrück aliliona wazo hilo kuwa zuri. Kwa kweli kilichotokea baada ya hapo ni aina ya maajabu ya ajira ambayo serikali ya Merkel hadi leo inaifaidika nayo, lakini sio Steinbrück. Ni kusema kwamba nyingi ya taratibu hizo zimetumiwa na waajiri. Leo kama asilimia 20 ya wafanyakazi wote wa Ujerumani wanapokea mishahara ambapo haiwatoshelezi kimaisha.
Steinbrück mgombea wa Ukansela kupitia chana cha SPD anasema kwa uyakinifu kwamba: "Kuna jambo limekwenda kombo kabisa. Jamii iko hatarini kugawika." Anataka kukabiliana na jambo hilo kwa dharura.
Steinbrück anapigania uchumi wa soko la kijamii ambao msingi wake ni kuwapa watu maisha mazuri kwa pamoja. Lakini wakosoaji wake wanasema mabadiliko hayo ya sera ya Steinbrück sio ya kuaminika yakiwemo malengo ya jamii aliyobuni ya kutaka kuweka kiwango cha chini cha mishahara kwa Ujerumani nzima.
Watu wanaofuatilia masuala ya uchaguzi wanasema upungufu wa uaminifu wa Steinbrück unatokana na nasaba yake binafsi. Mgombea huyo anatoka katika familia ya wafanyabisahara wa hali ya juu huko Hamburg na ni bwanyenye mno,lakini sio hayo tu yanayomuathiri.
Kampeni za uchaguzi zimekwenda kombo kuanzia mwanzo
Katika uchaguzi wa Ujerumani wa 2009 Kansela Angela Merkel na chama chake cha CDU na CSU pamoja na cha Kiliberali cha FDP alipata kura nyingi na kuweza kuongoza serikali bila ya chama cha SPD. Kufuatia uchaguzi huo Steinbrück alirudi kuwa mbunge wa kawaida na kutangaza kujitowa kwenye siasa za anga ya juu.
Badala yake alitunga kitabu kilichopata mafanikio na kupewa jina la Unterm Strich. Kitabu hicho kilikuwa juu ya wakati wake wa uongozi serikalini, shughuli zake akiwa profesa wa heshima katika vyuo vikuu ambapo amekuwa akilipwa malipo ya juu kwa kutowa hotuba akiwa kama mgeni wa heshima.
Hadi mwaka 2010 alikuwa hakufikiria iwapo atakuwepo tena kwenye siasa za ngazi ya juu na kushika madaraka lakini mambo yamekuja kuwa vengine kabisa.
Kwa takriban asilimia 94 amechaguliwa kwenye mkutano maalum wa SPD kuwa mgombea wa Ukansela katika uchaguzi mkuu wa Ujerumani mwa huu wa 2013.
Lakini furaha hiyo haikudumu kwa muda mrefu, kwani muda mfupi baada ya hapo ilikuja kubainika hadharani kwamba Steinbrück alilipwa zaidi ya euro milioni moja kutokana na mihadhara anayoitowa kwa benki na kampuni za ushauri wa fedha.
Baya zaidi, kwanza kabisa, aliiona hali hiyo kama ni suala la kibinafsi na kutolitolea taarifa kwa muda mrefu lakini hatimae alibainisha kila kitu hadharani. Zaidi ya hayo alikosowa mshahara wa kansela wa kipidi cha usoni kuwa ni mdogo sana na pia kusema yeye hanywi vileo vya bei rahisi. Mambo hayo yalimuathiri sana mgombea huyo mkuu wa SPD na yote hayo hayaowani na taswira ya mgombea wa chama hicho kwa watu wa hali ya chini.
Nyuma ya Merkel kwenye kura za maoni
Matokeo ya uchunguzi wa maoni yanaonyesha hawezi kumfikia Angela Merkel. Hata hivyo, Peer Steinbrück havunjiki moyo na hilo anaendelea kupambana na kusema “Hapo mwaka 2005 chama cha SPD kilionekana kufanya vibaya kabla ya uchaguzi lakini baadae kilijichomoza na kufanya vizuri."
Mgombea huyo wa Ukansela wa SPD wiki zilizopita kwa kweli alikuwa ameshughulika kuendelea kuunadi mpango wake wa kuongeza kodi kwa watu wa kipato cha juu, kuondowa dhuluma zote za kijamii katika nchi na kuwandeleza watu mbele zaidi.
Steinbrück hususan anataka kuwasadia wanawaKe wanaofanya kazi wapate mshahara sawa na wanaume, kuboresha matunzo ya watoto na mipango ya kustaafu.
Kwa maoni ya wafuasi wake mgombea huyo bado ana karata ya akiba inayoweza kumpatia ushindi kwani ni mtu thabiti anayeweza kuaminika akiwa kama mawanasiasa halikadhalika akiwa raia wa kawaida.
Steinbrück amefunga ndoa na mkewe ambaye ni mwalimu wa biolojia na siasa tokea miaka 38 iliopita na ni baba wa watoto watatu ambao hivi sasa tayari ni wakubwa.
Steinbrück haoni haja ya kumfanya Angela Merkel na chama chake cha CDU kuwa mshirika wake tena wa kisiasa. Hoja yake: " Bibi Merkel ameendelea tu kuitawala Ujerumani. Ameifanyia nchi usarifu mchache."
Kwa Steinbrück, chama anachopendelea kwa sasa kushirikiana nacho kuunda serikali ya mseto pindipo ushindi ni chama cha Kijani.
Mwandishi: Wolfgang Dick
Tafsiri: Mohamed Dahman
Mhariri: Mohammed Khelef