1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wasichana Uganda waozwa wanapokosa uwezo wa kununua Sodo

24 Oktoba 2017

Asilimia kubwa ya wasichana nchini Uganda wanalazimika kuolewa mapema kwasababu ya kukosa uwezo wa kununua vifaa vya kujihifadhi wakati wa hedhi ambavyo ni ghali mno nchini humo

https://p.dw.com/p/2mQTz
Tansania Mädchenschule Schülerinnen Afrika
Picha: Zuberi Mussa

Hali hii pia inaathiri masomo ya wasichana wengi wanaouvunja ungo kutokana na ukosefu wa vyoo dhabiti katika shule zao.

Kulingana na shirika la kimataifa la Aid Agency Plan, mamia ya wasichana wanalazimishwa kuozwa mapema na wazazi wao wachochole ambao hawana uwezo hata wa kuwanunulia bidhaa za usafi.

Cha kusikitisha zaidi ni kuwa wengi wanashinikizwa kufanya ngono na wavulana wanaojitolea kuwanunulia vifaa vya usafi kama malipo yao. Baadhi huishia kubeba mimba na kulazimika kukatiza masomo yao.  

Swala la hedhi ya kila mwezi kwa wasichana ambalo kwa kawaida ni mwiko kulizungumzia katika mazingira ya kihafidhina ya Uganda, liligonga vichwa vya habari mwaka huu wakati mwanaharakati mmoja wa swala hilo alipokamatwa na kuzuiliwa kwa kumtusi rais Yoweri Museveni katika mtandao wa kijamii wa facebook.

Mwanaharakati huyu kwa jina la Stela Nyanzi aliwashambulia rais Museveni na mkewe baada ya kushindwa kutimiza ahadi aliyoitoa wakati wa uchaguzi wa kugawa vifaa vya hifadhi ya hedhi kwa wanafunzi wa kike.

Mapema mwaka huu, mama wa taifa Janet Museveni ambaye ni pia ni waziri wa elimu amesema serikali haina fedha ya kutosha.

Hatahivyo mwanaharati huyo alizindua kampeni iitwayo pads4girlsug kukusanya mchango wa kununua vifaa vya kujihifadhi wakati wa hedhi  vitakavyosambazwa mashuleni. Aliachiliwa kwa dhamana mwezi Mei baada ya mwezi mmoja kizuizini na sasa anakabiliwa na shtaka la unyanyasaji mitandaoni.

Hata hivyo afisa mmoja wa serikali amesema wizara ya elimu inafanya mazungumzo na mashirika ya kutoa misaada na mashirika ya dawa kwa nia ya kutoa bure bidhaa za usafi kwajili ya wasichana wa shule.

Italien Kinder Zwangsheirat Amnesty
Muigizaji akiigiza kama muathirika wa ndoa za mapemaPicha: Getty Images/AFP/G. Bouys

Ndoa za Mapema kwa Wasichana

Kulingana na shirika la umoja wa mataifa la watoto UNICEF, Karibu asilimia 60 ya wasichana nchini Uganda wanakosa kwenda darasani kwasababu shule zao hazina vyoo vya kutosha na vifaa vya usafi vya kuwasaidia wasichana wakati wa hedhi. Hali hii inakatiza masomo ya wasichana wengi na kusababisha uwezekano mkubwa wa kuolewa.

Badala yake wasichana huishia kutumia vitambaa vibovu, majani yaliokauka, nyasi au karatasi kujikingia hedhi.

Japo taifa la Uganda limepiga marufuku ndoa za mapema, wane kati ya wasichana kumi wanaozwa kabla ya kufikisha miaka 18 na mmoja kati ya kumi kabla ya kufikisha miaka 15, kulingana na shirika la UNICEF.

Uganda sio nchi pekee inayotarajia  kutoa buretaulo za usafi kama njia ya kuongeza viwango vya elimu ya wasichana.Mataifa ya Kenya na Zambia pia wameahidi kusambaza vifaa hivyo vya hedhi kwa wanafunzi wa shule - ingawa shirika la kutoa msaada la WaterAid limesema  Zambia bado haijajihusisha kutoa fedha zozote.

Shinikizo limetolewa kwa serikali ya Uganda kupunguza gharama za bidhaa hizo kuhakikisha mashule yana vyoo vya kutosha na tofauti vya wasichana na kuanzisha masomo kuhusu maisha ya kiutu uzima kuondoa unyanyapaa unaowakabili wasichana. Haya yanajiri wakati ambapo viongozi tofauti barani Afrika wameungana kupambana na kumaliza ndoa za mapema katika maeneo ya magharibi na kati ya Afrika, maeneo ambayo yana idadi kubwa ya ndoa za mapema ulimwenguni.

Mwandishi: Fathiya Omar/RTRE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman