Wasichana milioni 700 walazimishwa kuolewa
11 Oktoba 2016Ripoti mpya ya shirika la Save the Children imesema kuwa ndoa za utotoni zinawakabili wasichana wadogo wengine wakiwa hata na umri wa miaka 10 pekee. Ripoti hiyo imeeleza kuwa takribani wasichana milioni 700 duniani kote walilazimishwa kuolewa huku wakiwa chini ya umri wa miaka 18. Inahofiwa kwamba kufikia mwaka 2050 huenda wasichana bilioni 1.2 wakaingizwa katika ndoa za utotoni huku umasikini na majanga ya vita yakitajwa kuwa ndio vyanzo vikuu vya mashaka haya yanayowapata baadhi ya watoto wa kike.
Kwa mujibu wa afisa mtendaji mkuu wa shirika la Save the Children, Bibi Susanna Krueger, watoto wa kike wanakabiliwa na hatari ya kudhulimiwa kimapenzi jambo linalowaweka kwenye hatari ya kuambukizwa maradhi ya ngono. Shirika hilo lisilo la kiserikali lina uwakilishi katika nchi 144 ambako kuna matatitzo mengi yanayomkabili mtoto wa kike na hasa katika maswala ya elimu, ndoa za utotoni, mimba za utotoni na vifo wakati wa uzazi.
Nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara zaongoza
Nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara zimetajwa kuwa ndio nchi zilizo na visa vingi vya mateso yanayowakumba watoto wa kike, huku Afghanistan, India, Yemen na Somalia zikiwa ni nchi zilizo na asilimia kubwa ya wasichana wanaokabiliwa na ndoa za utotoni.
Katika ripoti hiyo ya shirika la Save the Children, nchi za Magharibi, zikiwemo Marekani na Uingereza, zimetajwa kuwa na idaidi kubwa ya watoto wa kike wanaopata mimba wakiwa na umri mdogo.
Ujerumani imetajwa kuwa ni mojawapo ya nchi ambazo ndoa za wasichana walio chini ya umri bado zinafanyika ijapokuwa si kwa kiwango kikubwa.
Huku siku hii ya mtoto wa kike ikiwa inaadhimishwa katika Umoja wa Mataifa, shirikajingine linalo shughulika na maswala ya watoto la Plan International limesema kuwa idaidi ya wasichana wanaojiunga katika shule za msingi inaelekea kuwa sawa na ile ya wavulana, ingawa wasichana wengi hawakamilishi masomo yao. Takribani wasichana milioni 39 wenye umri wa miaka 11 hadi 15 hawamalizi masomo ya msingi.
Kwa mujibu wa shirika la Plan International ni kwamba mara nyingi wasichana wanapoendelea kukua, familia zinawashurutisha kuchangia kiuchumi kutokana na hali ngumu ya maisha hivyo basi wengi wa wasichana hao hulazimika kuacha masomo yao.
Tatizo hili limekuwa sugu hasa barani Afrika ambako matatizo mengi ya kimaisha yanachangia kwa wasichana kuacha shule pamoja na kuhusishwa watoto hao katika ndoa za lazima hata ingawa wengi wao huwa wana umri mdogo na vilevile wengine hupata mimba wakiwa bado wadogo.
Mwandishi: Zainab Aziz/DPAE
Mhariri: Mohammed Khelef