1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wasi wasi katika Raas ya Korea

8 Machi 2013

Hali ni ya wasi wasi katika raas ya Korea baada ya baraza la usalama la Umoja wa mataifa kuiwekea vikwazo serikali ya Korea ya kaskazini huku Pyongyang ikisitisha makubaliano yote pamoja na Korea ya kusini.

https://p.dw.com/p/17tQb
KIongozi wa Korea ya kaskazini Kim Jong-Un (kati)pamoja na wajumbe katika mkutano wa viongozi kuhusu usalamaPicha: KCNA VIA KNS/AFP/Getty Images

Taarifa hiyo imetangazwa na vyombo vya habari vya serikali,siku moja baada ya baraza la usalama la Umoja wa mataifa kuiwekea vikwazo nchi hiyo ya kikoministi baada ya kufanya jaribio la tatu la kinuklea na kutishia pia kuihujumu Marekani na Korea ya kusini kwa silaha za kinuklea.

Vyombo vya habari vya serikali ya Korea ya kaskazini vimeinukuu pia kamati inayoshughulikia Muungano wa Korea mbili ikisema "Pyongyang itabatilisha makubaliano yote ya kutoshambuliana" yaliyofikiwa kati ya Kaskazin i na Kusini."

Kituo cha mawasiliano kilichoko katika eneo lililotakaswa na silaha katika kijiji cha mpakani cha Panmunjom kitafungwa mara moja-taarifa hiyo imesema.

Ghadhabu za Pyonyang zimefuatia uamuzi wa baraza la usalama la Umoja wa mataifa kuiwekea vikwazo zaidi Korea ya kaskazini-nchi mojawapo inayokabwa na vikwazo vingi vya kimataifa.

China yahimiza utulivu

UN Sicherheitsrat Sanktionen Nordkorea
Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa laiwekea vikwazo zaidi Korea ya kaskazini.Picha: Reuters

Katika wakati ambapo vikwazo vya awali vinazungumzia marufuku ya silaha kwa Korea ya kaskazini,hivi vya sasa vinasitisha shughuli zote za fedha pamoja na wakorea ya kaskazini au makampuni yanayotuhumiwa kuisaidia nchi hiyo kuendeleza miradi ya kinuklea na makombora yenye uwezo wa kushambulia toka bara moja hadi jengine.

Vikwazo vipya vinaruhusu shehena katika meli zinazoelekea Korea ya kaskazini zikaguliwe,meli zisiruhusiwe kutia nanga na ndege pia za nchi hiyo zisiruhusiwe kupita katika anga za nchi zote za dunia.

Kipya safari hii ni kwamba hata washirika wakubwa wa Korea ya kaskazini, China wameunga mkono azimio hilo la baraza la usalama la umoja wa mataifa.

Hata hivyo balozi wa China katika Umoja wa mataifa Li Baodong anasema:"Kipa umbele kwa sasa ni kupunguza mvutano na kutuliza ghadhabu na kusaka ufumbuzi kwa njia za kidiplomasia."

Kwa upande wake balozi wa Marekani katika Umoja wa mataifa bibi Susan Rice anasema "ulimwengu mzima umesimama kidete kudai rasi ya Korea itakaswe na silaha za kinuklea."

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/dpa/AFP

Mhariri:Yusuf Saumu