1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Washukiwa wa mauaji ya watoto Njombe Tanzania wakamatwa

Deo Kaji Makomba30 Januari 2019

Serikali ya Tanzania imesema watu wanaoshukiwa kuwaua watoto eneo la Njombe kwa tuhuma za kishirikina wameshakamatwa. Watoto Sita waliuwawa na baadhi ya viungo vyao kukatwa.

https://p.dw.com/p/3CQUe
Tansania Mbagala Polizist vor Wahllokal
Picha: picture-alliance/AP Photo/Khalfan Said

Sakata la mauaji ya watoto wadogo katika mikoa ya kusini mwa Tanzania limeingia bungeni hii leo huku serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ikisema kuwa tayari wahusika wa matukio hayo ya kikatili wamekwishakamatwa. 

Kauli hiyo ya serikali ya Tanzania imetolewa hii leo bungeni mjini Dodoma na Waziri wa mambo ya ndani ya nchi Kangi Lugola, wakati akijibu swali la mbunge wa Mufindi Kaskazini Menrad Kigola, aliyetaka kujua serikali imechukua hatua gani kuhusiana na mauaji hayo ya kikatili  yaliyotokea katika mkoa wa Njombe uliopo kusini mwa Tanzania.

Mauaji hayo yamezua taharuki katika mikoa ya kusini mwa Tanzania, yanaelezwa kuwa ni ukatili mkubwa unaofanywa na watu wenye imani potofu za kishirikina. 

Siku za hivi karibuni kumeibuka vitendo vya kuuwawa watoto wadogo vinavyofanywa na watu wasiojulikana katika nyakati tofauti ambapo watoto Sita wenye umri kati ya miaka sita na mitatu waliuwawa na baadaye miili yao ilipatikana ikiwa imetolewa baadhi ya viungo kama meno, masikio, na viungo vya siri. Mauaji hayo yanahusishwa na imani za kishirikina.

Mwandishi: Deo Kaji Makomba/DW-Dodoma

Mhariri: Daniel Gakuba