1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Washukiwa kuandaa njama ya mapinduzi watiwa mbaroni Madagascar

19 Aprili 2010

Kisiwani Madagascar, watu 19 walikamatwa na vikosi vya usalama siku ya Jumapili, wakishukiwa kupanga kuipindua serikali, huku uvumi wa njama za mapinduzi ukienea nchini humo.

https://p.dw.com/p/N0Us
Image #: 7406492 (080321) -- ANTANANARIVO, March 21, 2009 (Xinhua) -- Andry Rajoelina, former opposition leader, is sworn in as the president of the High Transitional Authority of Madagascar during an official ceremony held at a stadium in central Antananarivo, capital of Madagascar, March 21, 2009. Andry Rajoelina called for national reconciliation in a speech he made during his inaugural ceremony. Xinhua /Landov
Rais wa Madagascar Andry Rajoelina.Picha: picture-alliance/ landov

Kwa mujibu wa mkuu wa vikosi vya usalama, Luteni Kanali Rene Lylison, washukiwa hao walipanga kuyashambulia makaazi ya waziri mkuu,alfajiri ya leo Jumatatu. Amesema, walikuwa na azma ya kuua na kuleta mgawanyo jeshini.

Nchini Madagascar watu wanazidi kuvunjika moyo na utawala wa Rais Andry Rajoelina,ambae hapo awali alikuwa meya wa mji mkuu Antananarivo. Yeye alishika madaraka mwezi wa Machi 2009 kwa msaada wa wanajeshi walioasi. Na Machi mwaka huu, kiongozi huyo na wafuasi wake wapatao 108 waliwekewa vikwazo na Umoja wa Afrika kwa sababu ya kushindwa kuunda serikali ya umoja wa taifa pamoja na vyama vitatu vikuu vya upinzani nchini humo.

Wachambuzi wanasema kuwa jeshini, baadhi ya maafisa wa ngazi za juu wamechoshwa na hali inayokutikana hivi sasa nchini humo, wakati Rajoelina akishindwa kuumaliza mgogoro wa kisiasa na kurejesha utawala wa kikatiba. Tarehe 12 mwezi huu, wakuu wa jeshi walimuarifu Rais Rajoelina kuwa anapewa muda, hadi mwisho wa mwezi huu wa Aprili, kuwasilisha mpango utakaoweza kumaliza mgogoro wa kisiasa na kuondosha hali ya wasiwasi inayowatisha wawekezaji wa kigeni na hivyo kuathiri uchumi wa nchi hiyo.

Baadhi ya wachambuzi wanasema, uamuzi huo wa jeshi labda ni hatua iliyohitajiwa kuchukuliwa ili kuyaleta pamoja makundi mbali mbali ya kisiasa katika meza ya majadiliano kumaliza ugomvi wao. Jeshi limegawanyika tangu vikosi vilivyoasi vilipomsaidia Rajoelina kujinyakulia madaraka. Sasa hata serikali yake imegawanyika.

Mapema mwezi huu, waziri mkuu wa serikali ya Rajoelina alimfukuza kazi Waziri wa Jeshi, Jemadari Noel Rakotonandrasana, katika hatua ya kutokuwa na imani nae. Lakini jemadari huyo amekataa kuacha wadhifa wake. Licha ya kukamtwa baadhi ya maafisa wa kijeshi na raia kadhaa, kwa sasa bado haijulikani nani aliehusika na njama inayotiliwa shaka kuwa ni ya mapinduzi.

Mwandishi: P.Martin/RTRE

Mhariri: M.Abdul-Rahman