Washirika katika vita vya Yemen wagombana
30 Agosti 2019Wakijibu tuhuma zinazodai kwamba wamewalenga wanajeshi wa serikali, vongozi wa mjini Abu Dhabi wamesema wamefanya hujuma hizo ili kujihami dhidi ya wanamgambo magaidi wanaotishia ushirika unaoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya waasi wa Houthi ambao Umoja wa Falme za Kiarabu ni mmojawapo wa washirika hao.
Taarifa ya wizara ya mambo ya nchi za nje imetangazwa Agosti 29 muda mfupi baada ya waasi wanaopigania kujitenga eneo la kusini mwa Yemen kuudhibiti upya mji wa Aden na kuwalazimisha wanajeshi wa serikali walioukomboa mji huo siku moja kabla, kutoroka.
Hujuma za ndege za kivita zilizofanyika jumatano na alkhamisi iliyopita "zimeyalenga makundi yenye silaha yanayoshirikiana na magaidi" viongozi wa Abu Dhabi wamesema wakimaanisha wafuasi wa itikadi kali wanaotuhumiwaq kuwa sehemu ya vikosi vya serikali ya Yemen.
Rais wa Yemen aiomba Saudi Arabia iingilie kati
"Opereshini zimefuatia ripoti za idara za upelelezi zinazosema kwamba wanamgambo wanajiandaa kufanya hujuma dhidi ya vikosi vya serikali-taarifa ya wizara ya mambo ya nchi za nje imesema.
Serikali ya Yemen inayotambuliwa na jumuia ya kimataifa imeutuhumu Umoja wa falme za kiarabu kuwasaidia waasi wanaotaka kujitenga na kufanya hujuma za angani zilizoangamiza maisha ya wapiganaji 40 na kuwajeruhi raia 70.
Rais wa Yemen anaeishi uhamishoni nchini Saudi Arabia, Abd Rabbo Mansur Hadi ameitolea wito Saudi Arabia iingilie kati na kukomesha uungaji mkono wa Umoja wa Falme za kiarabu kwa waasi wanaopigania kujitenga eneo la kusini la Yemen.
Juhudi za upatanishi zinashika kasi
Waziri wa dola anaeshughulikia siasa ya nje ya Emirati Anwar Gargash amezitolea wito pande zote zirejee katika meza ya mazungumzo yanayosimamiwa na Saudi Arabia mjini Jeddah.
Wakati huo huo waziri wa mambo ya nchi za nje wa Sweeden Margot Wallstrom anapanga kuzitembelea Saudi Arabia, Falme za nchi za kiarabu, Oman na Jordan kuanzia jumaamosi ya Agosti 31 kwa lengo la kuzungumzia mzozo wa Yemen. Atakutana pia na wawakilishi wa serikali ya Yemen na mwakilishi wa Umoja wa Mataifa inaeshughulikia suala la Yemen.
Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/dpa/AFP
Mhariri: Grace Patricia Kabogo