Washington:Marekani yawataka washirika wake NATO kujihusisha zaidi Afghanistan
28 Novemba 2006Marekani amewataka washirika wake katika Jumuiya ya kujihami ya magharibi NATO ,wachukuwe juhudi zaidi kuhusiana na Afghanistan. Wito huo wa Marekani umetolewa kabla ya kuanza mkutano wa viongozi wa jumuiya hiyo unaoanza leo katika mji mkuu wa Latvia-Riga . Wanachama wa NATO zikiwemo Ujerumani, Uhispania na Ufaransa wanakabiliwa na shinikizo la kuwataka wapeleke wanajeshi wao walioko katika jeshi la kimataifa nchini Afghanistan, katika eneo tete la kusini mwa nchi hiyo, ili kuwasaidia wanajeshi wa Uingereza, Canada na Uholanzi wanaopigana na waasi wa Taliban katika sehemu hiyo. Wito huo umekuja baada ya bomu la kujiripua kwa kujitoa mhanga kuwauwa wanajeshi wawili wa Canada katika mji wa kusini wa Kandahar, na kuifanya idadi ya wanajeshi wa kigeni waliouwawa mwaka huu kufikia zaidi ya 150. Ujerumani imesema kwamba wanajeshi wake 2,800 wana jukumu la kubakia kaskazini mwa Afghanistan.
Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Franz Josef Jung anasema la muhimu katika kuleta mafanikio ni kuboresha hali za maisha za Wa-afghan, na sio kuongeza idadi ya wanajeshi wa NATO ili kupambana na waasi.