1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WASHINGTON : Uturuki yatakiwa isivamie Iraq kaskazini

18 Oktoba 2007
https://p.dw.com/p/C7Ep

Marekani na washirika wengine wa mataifa ya magharibi pamoja na serikali ya Iraq wameitaka Uturuki kuepuka kuchukua hatua ya kijeshi kaskazini mwa Iraq baada ya bunge la nchi hiyo kutowa idhini hapo jana ya kushambuliwa kwa waasi wanaotaka kujitenga wa Kikurdi waliopiga kambi huko.

Muswada huo umeungwa mkono hapo jana na takriban vyama vyote vilioko bungeni isipokuwa kundi dogo la Wakurdi.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Washington juu ya suala Rais George W. Bush wa Marekani amesema wanaweka wazi kabisa kwa Uturuki kuwa hawafikiri ni kwa maslahi yao kutuma vikosi nchini Iraq na kwamba kwa kweli tayari wana wanajeshi waliowaweka nchini Iraq kwa muda sasa kwa hiyo hadhani itakuwa ni kwa maslahi ya Uturuki kutuma wanajeshi zaidi nchini humo.

Tokea miaka ya 1990 Uturuki imeweka idadi ndogo ya vikosi vyake katika maeneo ya mipakani ya kaskazini mwa Iraq ambapo waasi wa Kikurdi wamekuwa wakifanya mashambulizi mashariki mwa Uturuki katika kampeni ya kuwania uhuru wa jimbo lao.

Kuongezeka kwa mauaji yanayofanywa na waasi hao wa Chama cha Wafanyakazi wa Kikurdi PKK katika miaka ya hivi karibuni yamemuweka chini ya shinikizo Waziri Mkuu wa Uturuki Tayyip Recep Erdogan kuanzisha operesheni kubwa ya kijeshi ambayo Marekani inahofu inaweza kusababisha machafuko kwenye eneo hilo.

Umoja wa Ulaya umesisitiza matumaini yake kwamba Uturuki iheshimu haki ya kujitawala ya Iraq.

Makamo wa Rais wa Iraq Tareq al- Hashemi alikuwapo Uturuki kujaribu kutuliza mvutano huo.