Washington. Rais Bush ashutumu upanuzi wa makaazi ya Wayahudi katika ukingo wa magharibi.
13 Aprili 2005Waziri mkuu wa Israel Ariel Sharon jana alifanya mazungumzo na makamu wa rais wa Marekani Bwana Dick Cheney siku moja baada ya mkutano kati ya viongozi wa Marekani na Israel ambao ulionyesha tofauti kubwa kati ya washirika hao , kuhusiana na upanuzi wa makaazi ya Wayahudi katika ukingo wa magharibi.
Kiongozi mmoja katika ujumbe wa Israel amewaambia waandishi wa habari kuwa katika mkutano huo uliochukua saa moja na nusu, viongozi hao wawili walijadili masuala muhimu yanayohusu Israel na Marekani. Pia amesema viongozi hao wamejadili suala la uwezekano wa Iran kuwa na silaha za kinuklia, lakini hakutoa taarifa zaidi.
Mkutano huo umefanyika siku moja baada ya rais George Bush wa Marekani kuwa na mazungumzo na waziri mkuu wa Israel Ariel Sharon katika shamba lake huko Texas , mazungumzo yaliyolenga katika mipango ya Israel ya kujiondoa kutoka ukanda wa Gaza, lakini pia yalishuhudia rais huyo wa Marekani akimshutumu Bwana Sharon kwa mipango yake ya upanuzi wa makaazi ya wayahudi katika eneo la ukingo wa magharibi.
Maafisa wa Israel walitarajia kuwa suala hilo litawekwa kando baada ya kutokea ghasia katika eneo la kusini kwa ukanda wa gaza mwishoni mwa wiki.