WASHINGTON: Marekani yakosoa kilimo cha mipopi nchini Afghanistan
22 Mei 2005
Maafisa wa Marekani wamemtuhumu rais Hamid Karzai wa Afghanistan kuwa yeye kwa sehemu fulani anabeba jukumu la kushindwa kwa jitahada za kukomesha uzalishaji wa mipopi nchini Afghanistan.Gazeti la Marekani,New York Times,limenukulu barua iliyotumwa na ubalozi wa Marekani mjini Kabul mapema mwezi huu kwa waziri wa kigeni wa Marekani Condoleezza Rice.Barua hiyo imesema kuwa maafisa wa Afghanistan wa ngazi ya juu ikiwa ni pamoja na rais Karzai,hawakuchukua hatua za kutosha katika wilaya,kukabiliana na maafisa wa Kiafghanistan wanaopinga mradi unaosimamiwa na Marekani kukomesha uzalishaji wa mipopi.Hati hiyo vile vile imesema kuwa wafanyakazi wa Kingereza wanaoamua maeneo ya kuzituma timu za kupambana na uzalishaji wa mipopi,hawakuwa tayari kuimarisha juhudi hizo katika maeneo yenye uzalishaji mkubwa wa mipopi.Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa,mipopi ya Afghanistan mwaka uliopita,ilichangia zaidi ya asili mia 80 ya heroini duniani.