1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WASHINGTON: Korea ya kaskazini na Iran zatolewa mwito wa kufanyika mazungumzo juu ya nyuklia

24 Oktoba 2006
https://p.dw.com/p/CCzk

Kiongozi wa shirika la Umoja wa mataifa la kudhibiti nguvu za kinyuklia, Mohammed El Baradei, amezitolea mwito Korea ya kaskazini na Iran kufanyika mazungumzo juu ya sera za nchi hizo kuhusu nyuklia. Akizungumza akiwa mjini Washington nchini Marekani, Mohammed El Baradei, ameonya pia kuwa kuwekewa vikwazo nchi hizo huenda kukazichochea zaidi kubaki katika msimamo mkali.Amesema haamini Iran inatengeneza silaha za kinyuklia na kwamba kuna uwezekano wa kufikia mkataba na Korea ya kaskazini juu ya mpango wake wa kinyuklia.

Umoja wa mataifa ulipitisha kwa kauli moja azimio la kuiwekea vikwazo Korea ya kaskazini kufuatia jaribio lake la kuripua bomu la kinyuklia tarehe 9 Oktoba.

Huenda Iran nayo ikakabiliwa na vikwazo kutokana na kukaidi amri ya Baraza la usalama la Umoja wa mataifa inaoitaka nchi hiyo kusimamisha kurotubisha madini ya uranium.