WASHINGTON: Bush na Schroeder kujadili mageuzi ya Umoja wa Mataifa
26 Juni 2005
Rais George W.Bush wa Marekani na Kansela wa Ujerumani,Gerhard Schroeder watakutana siku ya jumatatu mjini Washington.Majadiliano yao yanatazamiwa kuhusika hasa na hatima ya Umoja wa Ulaya,msaada kwa mataifa yalio masikini na pia mageuzi katika Umoja wa Mataifa.Ziara ya Schroeder nchini Marekani inafanywa wiki mbili kabla ya viongozi hao kuhudhuria mkutano wa kilele wa madola saba tajiri yenye viwanda pamoja na Russia.Mkutano huo wa G8 utakaofanywa Scotland utazingatia hasa mabadiliko ya hali ya hewa na msaada kwa nchi za Kiafrika.Msemaji wa Ikulu ya mjini Washington,Scott McCllelan amesema ziara ya Schroeder nchini Marekani,inawapa viongozi hao nafasi nzuri ya kuzungumzia njia ya kuendelea kuimarisha uhusiano kati ya pande mbili.Bush na Schroeder walikutana mara ya mwisho ana kwa ana,mwezi wa February mwaka 2005 katika mji wa Mainz nchini Ujerumani.