WASHINGTON: BUSH ASIKITIKA KWA BERLUSCONI
5 Machi 2005Rais George W.Bush wa Marekani amempigia simu waziri mkuu wa Italia,Silvio Berlusconi kueleza majuto yake baada ya risasi zilizofyetuliwa na wanajeshi wa Kimarekani kumuuwa ajenti wa idara ya upelelezi ya Italia na kumjeruhi mwandishi habari,nje ya mji mkuu wa Iraq,Baghdad.Rais Bush amesema tukio hilo litachunguzwa kwa ukamilifu. Kwenye kituo cha ukaguzi cha jeshi la Kimarekani,risasi zilifyetuliwa ripota Guiliana Sgrena alipokuwa akishindikizwa,baada ya kuachiliwa huru na watekanyara wake.Ripota Sgrena aliejeruhiwa alipokea matibabu katika hospitali mjini Baghdad.Mwandishi habari huyo alitekwa nyara Februari 4 alipokuwa akifanya mahojiano barabarani karibu na Chuo Kikuu cha Baghdad.Italia kama mshirika wa Marekani ina wanajeshi 3,000 nchini Iraq.