Miradi ya India, Bangladesh, Iran na Ujerumani yashinda
4 Mei 2016Zaidi ya miradi 2300 iliyoandikwa katika lugha 14 kutoka duniani kote iliwasilishwa katika mashindano ya mwaka huu. Washindi walitangazwa katika vipengele vinne.
Washindi hao kwa mwaka 2016 ni kama ifuatavyo;
Mabadiliko ya Kijamii; Kampeni ya kusimamisha mashambulizi ya Tindikali nchini India
Uandishi wa habari wa masuala ya kiraia, ikiwa niFilamu ya" Razor's Edge" kutoka Bangladesh
Teknolojia kwa manufaa; Programu ya Gershad kutoka Iran
Sanaa na Utamaduni: Kuhusu kituo cha siasa nchini Ujerumani
Mabadiliko ya Kijamii
Mradi huu wa kampeni ya kusimamisha mashambulizi ya tindikali umeshinda tuzo katika kipengele cha mabadiliko ya kijamii .Unalenga kuwasaidia wanawake ambao ni wahanga wa mshambulizi ya Tindikali na ambao hujikuta wapweke na kubaguliwa kwa sababu ya miiko ya vurugu zilizofanywa dhidi yao. Mradi huo umefanikiwa kuanzisha eneo la kukutana, Sheroes Hangout linaendeshwa na manusura wa mashambulizi ya Tindikali na kutetea haki zao, kwa kutaka sheria zizuie mashambulizi na huduma za afya zitolewe kwa wahanga.
" Inaonekana kuleta mabadiliko kweli ya kijamii, na ukweli ni kwamba mradi huu umesaidia kuleta tofauti katika sheria" anasema Abhinandan Sekhri, mmoja ya wajumbe wa jopo la majaji wa Lugha ya Kihindi akimaanisha upigwaji marufuku ya uuzaji wa tindikali nchini humo.
Anaendelea kusema kuwa "Katika maeneo kama India, ambapo suala la jinsia limefunikwa na mfumo dume, kampeni kama hii lazima ipate ushindani mkubwa, kwasababu wanashinda wanawahamasisha wengine".
Uandishi wa habari za kiraia
Filamu ya"Razor's Edge"imeshinda tuzo katika kipengele cha uandishi wa habari za Kiraia. Filamu hii inaonyesha mazingira hatarishi yanayowapata waandishi wa habari za kimtandao"Bloggers"na waandishi wengine nchini Bangladesh na serikali kushindwa kukabiliana na ongezeko la mauaji yanayofanywa na watu wenye misimamo mikali ya dini ambapo katika kipindi cha wiki tano zilizopita tayari waandishi wanne wameuawa.
" Ukiwa katika nchi ambayo serikali inaonekana kutojali , inakuwa ni jukumu la raia kusimama peke yake na kudai haki, na ndicho ambacho filamu imeonyesha" anasema mjumbe wa jopo kutoka Bangladesh Rafida Bonya Ahmed ambaye alinusurika shambulizi mwaka 2015 lilipoteza maisha ya mume wake Avjit Roy.
" Inaonekana dhahiri kuwa serikali inahamasisha suala la kutoadhibiwa" ameongeza . " Ni mfano mzuri wa namna ya kuongeza uelewa ili kulinda haki za jamii kubwa nchini Bangladesh."
Tech for good: Teknolojia kwa manufaa
Sheria kali nchini Iran zinatoa mwelekeo, hususan kwa wanawake ni kitu gani wanapaswa kuvaa hadharani na polisi wa wanaposimamia utekelezaji wa misingi ya dini wanaingia katika mitaa kuhakikisha sheria hizo zinafuatwa. Programu hii ya simu za smartphone ya Gershad inategemea vyanzo kutoka katika makundi ya watu yanayowalenga polisi na njama zao na kuonekana katika ramani kwa nia ya kuwaamsha watu ili wawakwepe na kuendelea na shughuli zao.
"Programu hii ni muhimu kwasababu inaweza kuwasaidia watu, na pia kuonyesha hatua za kikandamizaji zinazochukuliwa na serikali ya Iran dhidi ya watu wake, na inaonyesha kuwa raia wa Iran hawana chaguo" anasema mjumbe wa jopo la majaji Golnaz Esfandiari akiongeza kuwa mamilioni ya watu wametiwa hatiani au kukandamizwa na polisi wa Iran .
Mmoja wa waanzilishi wa programu hii anasema " ni mwanzo wa mazungumzo kuhusu tabia za polisi hao na jitihada za kuimarisha haki za kiraia".
Sanaa na Utamaduni
Mradi wa Kijerumani wa kituo cha siasa ulishinda tuzo katika Sanaa na Utamaduni. Sanaa yake imejikita katika uandaaji wa matukio mbalimbali yakiwemo maandamano ya kuwasaidia wakimbizi na maandamano ya kupinga mauzo ya silaha za Ujerumani nchi za nje .
" Kwa miaka kadhaa kituo hiki kimekuwa na mada tofauti", anasema mjumbe Katharina Nocun . "Ni njia ya kupanua uwezo na kuangalia matatizo ya kimataifa yanavyoowanisha".
Washindi wote wa tuzo hizo wataalikwa katika sherehe kubwa wakati wa mkutano wa kimataifa wa DW kuhusu vyombo vya habari mwezi Juni. Taarifa zaidi kuhusu washindi hao wote zinapatikana katika tovuti ya www.thebobs.com
Mwandishi; Sylvia Mwehozi
Mhariri; Mohamed Abdul-Rahman