Washindi wa kupiga picha bora za wanyama pori mwaka 2020 watangazwa
Kila mwaka, makavazi ya kihistoria ya London huwatuza wapiga picha ambao wamenasa picha nzuri za mandhari. Hizi ni baadhi ya picha bora zilizoivutia zaidi DW.
Na mshindi ni...
Mshindi wa tuzo ya mpiga picha bora wa mwaka 2020 ni Sergey Gorshkov kutoka Urusi, aliyenasa picha ya chui milia aina ya Amur akiukumbatia mti wa Manchuria katika eneo la Mashariki mwa Urusi. Aina hiyo ya chui milia ambao pia wanafahamika kama chui wa Siberia wanapatikana tu katika eneo hilo. Ilimchukua mpiga picha Gorshov miezi 11 kunasa picha hiyo.
Picha ya kuonyesha hali ya utulivu
Nani asiyependa picha nzuri ya tumbili? Majaji walifurahishwa na picha ya Mogen Trolle ilimuonyesha tumbili wa aina ya proboscis mwenye pua ndefu akiota jua. Picha hii ilishinda kitengo cha "Portrait"-ambacho inaonyesha picha ya mnyama hadi shingoni. Tumbili wa aina hii wako katika hatari ya kuangamia na wanapatikana Kusini Mashariki mwa kisiwa cha Borneo na viunga vyake.
Uamuzi mgumu
Kuamua ni picha gani bora na yenye mvuto zaidi sio jambo rahisi- Majaji walikagua picha 49,000 kutoka kila pembe ya dunia. Ni mara ya kwanza katika historia ya miaka 56 ya mashindano hayo ambapo washindi walitangazwa kupitia matangazo ya moja kwa moja mtandaoni. Songda Cai alishinda kitengo cha picha zilizopigwa ndani ya maji kwa kunasa picha ya ngisi mwenye rangi ya dhahabu.
Maonyesho ya wazi
Mashindano hayo yanalenga kuangazia aina maalum ya wanyama duniani, mfano ni kama picha ya chura huyu aina ya Manduriacu anayepatikana tu katika eneo dogo la Ecuador. Mpiga picha Jaime Culebras alimnasa chura akining'inia katika tawi wakati wa mvua. Culebras aliibuka mshindi katika kitengo cha wanyama wenye kutambaa na kuishi nchi kavu na majini.
Uzuri wa asili
Picha hii inaonyesha nguvu kubwa iliyo nayo dunia. Mpiga picha Luciano Gaudenzio aliibuka mshindi katika kitengo cha mazingira. Picha zote zilizoshinda katika vitengo mbalimbali zitaonyeshwa katika makavazi ya kihistoria ya London kuanzia Oktoba, 16, 2020 hadi Juni 6 mwaka 2021. Waandalizi wanatumai kuwa, picha hizo zitatoa fursa kwa watazamaji kutafakari, na kupigania uhifadhi wa mazingira.
Binadamu wamo pia
Picha hii inamuonyesha tumbili mdogo akiwa amefungwa minyororo katika soko la ndege la Bali baada ya kunaswa msituni na kuuzwa. Paul Hilton alishinda kitengo cha wanyamapori kwa kuangazia biashara ya unyanyasaji wa wanyama pori. Washindi wanaangazia athari za binadamu kwa mazingira; tumbili aina ya macaque wanaweza kuuzwa na aghalabu hujipata katika hali ngumu.
Talanta yenye kuonyesha matumaini
Mshindi wa kitengo cha mpiga picha mwenye umri mdogo wa kati ya miaka 15-17 ni Liina Heikkinen kutoka Finland aliyenasa picha ya mbweha akila windo lake la bata. Mbweha huyo anajificha ili asigawe windo hilo kwa wenzake. Ni sehemu moja ya historia iliyonaswa vizuri kwenye picha, alisema jaji Shekar Dattatri.
Mshindi mwenye umri mdogo zaidi katika mashindano
Mustakabali wa mpiga picha Sam Sloss unang'aa. Picha yake ya samaki iliyopewa jina "A mean mouthfull" yaani mdomo bahili ilitawazwa mshindi katika kitengo cha wapiga picha wenye umri wa kati ya miaka 11-14. Sloss alitamaushwa na jinsi mdomo wa samaki huyo ulivyokuwa wazi.
Jirani wanaoruka
Kushinda kitengo cha wanyama wasiokuwa na uti wa mgongo, Frank Deschandol amenasa wadudu aina ya nyigu wakiingia katika viota vyao. Wadudu hao, ambao kawaida hawaingiliani, walinaswa kwa kutumia mbinu ya kipekee ya upigaji picha kasi. Picha hiyo ilinaswa katika eneo la Normandy, Ufaransa.
Naswa kwenye kamera
Picha hii ya paka aina ya Pallas ambao pia wanajulikana kama manuls, ilipigwa katika mlima wa Qinghai-Tibet ulioko Kaskazini magharibi mwa China. Mpiga picha Shanyuan aliwafwatilia paka hao walipokuwa wanatafuta chakula. Katika picha, paka hao wanaitwa na mama yao baada ya kuonekana kwa mbweha karibu.