WARSAW; Rais Köhler atoa hotuba kuadhimisha miaka 25 ya chama cha wafanyakazi cha Solidarity
31 Agosti 2005Rais Horst Köhler wa Ujerumani leo ametoa hotuba katika kiwanda cha uhandisi wa meli mjini Gdansk nchini Poland.
Ameitumia hotuba yake kumulika mchango wa Poland katika kuporomoka ukuta wa chuma na kuungana upya Ujerumani.
Rais Köhler alikuwa anahutubia katika sherehe ya kuadhimisha miaka 25 tangu kuundwa kwa chama cha wafanyakazi wa Poland Solidarity.
Wakiongozwa na fundi umeme Lech Walesa, wafanyakazi waliokuwa wakigoma katika kiwanda cha uhandisi wa meli cha Gdansk, walibuni chama cha kwanza huru cha wafanyakazi wa Ulaya Mashariki mnamo siku kama ya leo katika mwaka 1980.
Katika kipindi cha miezi michache iliyofuatia mamilioni ya wafanyakazi walijiunga na chama cha Solidarity na miaka kumi baadae Lech Walesa akachaguliwa kuwa rais wa Poland.
Wakati huo huo chama cha SPD kimefanya mkutano wake maalum mjini Berlin na kansela wa Ujerumani Gerhard Shröder amesema kwamba ana matumaini ya kushinda katika uchaguzi ujao licha ya kura ya maoni kuonyesha kuwa chama kikuu cha upinzani CDU kinaongoza kwa asilimia 40.