1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WARSAW/LONDON:Hatua ya Uingereza ya kughairisha kura ya maoni juu ya katiba ya Ulaya haijaimaliza katiba hiyo asema Adam Rotfeld

6 Juni 2005
https://p.dw.com/p/CF6G

Waziri wa mambo ya nje wa Poland Adam Rotfeld amesema katiba ya Umoja wa Ulaya bado iko imara licha ya mipango ya Uingereza ya kughairi kura yake ya maoni juu ya katiba hiyo.

Waziri huyo ameyasema hayo katika mkutano huko Warsaw na maafisa wakipoland kujadili juu ya suala hilo la katiba ya Umoja wa Ulaya. Amesema ilichofanya Uingereza ni kughairisha tu mpango huo lakini bado hawajaikataa katiba hiyo kwa hiyo katiba hiyo itaendelea kuwepo.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Uingereza bwana Jack Straw ametangaza rasmi bungeni kwamba serikali ya Uingereza imeamua kusimamisha mipango yake ya kuandaa kura ya maoni ili kutoa nafasi zaidi ya katiba hiyo kujadiliwa.

Hatua hiyo imefuatia kukataliwa kwa katiba hiyo katika nchi za Ufaransa na Uholanzi wiki iliyopita,na kusababisha uungwaji mkono wa katiba hiyo kuzoroteka katika mataifa mengine ya Umoja huo.

Hata hivyo Kansela wa Ujerumani Gerhard Schoeder na rais wa Ufaransa Jacque Chiraq wamesisitiza kwamba harakati za kuiidhinisha katiba hiyo lazima ziendelee katika mataifa yote wanachama wa umoja huo. Viongozi wa Umoja huo wanajitayarisha kwa mkutano wa kilele wiki ijayo kujadili jinsi ya kuendelea. Uingereza itachukua uongozi wa Umoja huo wa wanachama 25 mwezi July.