1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapinzani Zimbabwe wafikishwa mahakamani

Isaac Gamba
5 Agosti 2018

Wanachama kadhaa wa chama cha upinzani nchini Zimbabwe (MDC) wamefikishwa mahakamani Jumamosi wakikabiliwa na mashitaka ya kufanya vurugu baada ya uchaguzi wa Jumatatu.

https://p.dw.com/p/32dTE
Simbabwe Präsidentschaftswahl Inhaftierung Oppositioneller
Picha: picture-alliance/AP Photo

Wanachama hao  wanaodaiwa kufanya vurugu katika ofisi za chama tawala pamoja na kuchoma moto magari wamerejeshwa mahabusu hadi ombi lao la kupata dhamana litakaposikilizwa kesho Jumatatu. Kiasi watu sita walifariki dunia baada ya wanajeshi kuwafyatulia risasi waandamanaji hatua iliyokumbusha kumbukumbu ya vurugu baada ya uchaguzi wakati wa utawala wa Robert Mugabe.

 Mnangagwa amekishutumu chama  cha Movement for Democratic Change- MDC kwa kusababisha vurugu na kuahidi kuunda tume huru kuchunguza mauaji hayo. Tume ya uchaguzi  ilimtangaza Mnangagwa kushinda uchaguzi kwa asilimia 50.8 ya kura dhidi ya mgombea wa MDC Nelson Chamisa aliyepata asilimia 44.3 ya kura.

Mnangagwa mshirika wazamani wa rais Robert Mugabe ametoa mwito wa mshikamano  ikiwa ni baada ya mshindani wake katika kuwania urais Nelson Chamisa wa chama cha MDC kuyakataa matokeo akisisitiza alikuwa ndiye mshindi katika uchaguzi.

 Wakili wa upande wa utetezi Denford Helimani amesema wanaume 16 pamoja na wanawake wanane wamekamatwa ikiwa ni hatua dhidi ya upinzani.

Mnangagwa asisitiza uchaguzi ulikuwa huru na haki

Simbabwe Präsidentschaftswahl Emmerson Mnangagwa erklärter Wahlsieger
Rais wa Zimbabwe Emmerson MnangagwaPicha: Getty Images/D. Kitwood

Mnangagwa amekuwa akisisitiza  kuwa uchaguzi wa Jumatatu ulikuwa huru na haki na kuusifia uchaguzi  kuwa ni mwanzo mpya mnamo wakati akichukua hatua kukomesha kutengwa kwa Zimbabwe na Jumuiya ya kimataifa.

Waangalizi wa kimataifa wameusifu uchaguzi huo kuwa umefanyika kwa amani  ingawa waangalizi wa Umoja wa Ulaya wanasema Mnagagwa alitumia taasisi za serikali pamoja na vyombo vya habari kushinda uchaguzi kutokana na kampeni za uchaguzi huo kutofanyika katika mazingira sawa ya huru na haki.

Chamisa mchungaji na mwanasheria mwenye umri wa miaka 40 ametoa mwito kwa wafuasi wake kujiepusha na vurugu wakati akitarajia kupinga matokeo ya uchaguzi  mahakamani.

Mnangagwa aliye na umri wa miaka 75 anasema Chamisa yuko huru kupinga matokeo hayo ya uchaguzi mahakamani  ingawa hatua hiyo inaonekana kupewa nafasi kidogo kubadilisha matokeo.

Mshirika huyo wazamani wa Robert Mugabe alichaguliwa kuongoza chama cha ZANU-PF baada ya Mugabe kujizulu Novemba mwaka jana kufuatia shinikizo la jeshi baada ya kukaa madarakani miaka 37.

 Makundi ya haki za  binadamu yameonesha wasiwasi kuwa hatua ya polisi kutumia nguvu zaidi dhidi ya waandamanaji ni dalili ya jinsi anavyotarajia kutawala nchini humo.

Mwandishi: Isaac Gamba/AFPE

Mhariri : Sekione Kitojo