Wapinzani waungana kumng'oa Mosile Lesotho
30 Mei 2012Kiongozi wa chama cha All Basotho Convention (ABC) Tom Thabane alisema jana jioni kuwa vyama vitano vimekubaliana kuunda ushirikiano ambao utavipa angalau viti 64 kati ya jumla ya viti 120 vya bunge la Lesotho. Thabane alisema lengo llao ni kuleta demokrasia ya kweli nchini Lesotho lakini kwa vile hakuna chama kinachoweza kuunda serikali kivyake, hawana budi kuunganisha nguvu zao kufanikisha azma hiyo.
Matokeo rasmi kutoka katika uchaguzi wa Jumamosi iliyopita yalionyesha kuwa chama cha Democratic Congress cha Waziri Mkuu Mosili kilishinda viti 48 ambapo viti 41 ni vya kuchaguliwa na viti 7 ni maalum kutokana na ushindi wa ujumla. Lakini ushindi huu hauwezi kukisaidia chama hiki kuunda serikali kivyake na hivyo kuna haja ya ushirikiano.
Uchaguzi wa Jumamosi ndiyo ulifuatiliwa kwa karibu zaidi katika miaka 14 wakati kuchaguliwa kwa Mosili kulipozusha ghasia na kuua watu 100, jambo lililolaazimu majeshi ya mataifa jirani kuingilia kati kutuliza hali. Kama chama Kikubwa zaidi, Democratic Congress kinakuwa na haki ya kwanza kujaribu kuunda serikali ya Umoja wa kitaifa lakini matumaini hayo yanaonekana kufifia kufuatia hatua ya vyama vya upinzani.
Mosili moja ya viongozi wanaodharauliwa zaid Afrika
Kura ya maoni iliyoendeshwa mwezi uliyopita ilimuweka Waziri Mkuu Mosili miongoni mwa viongozi watano wanaodharauliwa zaidi barani Afrika akiwa na asilimia 39 tu ya kukubalika kwa kazi yake, na hivyo kuwekwa katika kapu moja na watu kama rais Mugabe wa zimbabwe. Mosili mwenye umri wa miaka 67 alisema wakati wa kampeni kuwa atakabidhi madaraka kama atashindwa.
Chini ya makubaliano ya vyama vya upinzani, chama cha Lesotho Congress for Democracy (LCD) kitajumulisha viti vyake 26 na vile 30 vya ABC wakati vyama vidogo vya Basotho National Party, Popular Fund for Democracy na Marematlou Freedom Party navyo vitaungana nao. Viongozi kutoka vyama vyote vitano walikuwepo wakati tangazo hilo likitolewa ambapo walisema kuwa muundo wa serikali ya mseto utabainishwa hapo baadae.
Chini ya mfumo wa uchaguzi mchanganyiko katika utawala wa kikatiba katika Falme ya Lesotho, wapiga kura huchagua wabunge kuwakilisha majimbo 80. Viti vingine 40 vinakuwa maalum na vinatolewa chini ya mfumo wa ulinganifu.
Miaka 14 ya utawala
Mosisili aliingia madarakani mwaka 1998 kama kiongozi wa chama cha LCD lakini alijitenga na chama hicho na kuanzisha chama cha Democratic Congress Machi mwaka huu baada kutokea kutoelewana na viongozi wengine kufuatia nia yake ya kutaka kujichagulia mrithi.
Ugomvi wa binafsi baina ya viongozi wakuu watatu wa vyama ambao wote waliwahi kuwa wanachama wa LCD ulitawala uchaguzi katika taifa hilo ambapo zaidi ya nusu ya wakaazi wake milioni mbili wanaishi katika umaskini.
Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga\AFPE
Mhariri: Mohammed Abdul Rahman