Wapiganaji washirika wa Urusi wauawa nchini Syria
16 Februari 2018Muda zilipotolwa taarifa za vifo hivyo unawiana na mapigano ya Februari 7, karibu na mji wa Deir al-Zor nchini Syria ambako kwa mujibu wa maafisa wa Marekani na washirika wa wapiganaji waliohusika , majeshi ya muungano yanayoongozwa na Marekani yalishambulia vikosi vinavyoshirikiana na Urusi ambayo ni mshirika wa rais wa Syria Bashar al- Assad.
Maafisa wa Urusi wanasema raia watano wanaweza kuwa waliuawa lakini hawana mahusiano na vikosi vya urusi.
Mapambano hayo yanaonesha kuwa Urusi inajihusisha zaidi kijeshi nchini Syria kuliko inavyosema na kuna uwezekano ikaingia katika makabiliano na Marekani nchini Syria.
Idadi hiyo ya vifo ndiyo kubwa zaidi katika mapambano ya mara moja tangu wakati wa mapambano makali nchini Ukraine mwaka 2014 yaliyosababisha vifo vya wapiganaji 100. Hata hivyo Urusi imekuwa ikikanusha kupeleka wanajeshi na wapiganaji wa kujitolea nchini Ukraine na haijawahi kuthibitisha idadi hiyo.
Kwa mujibu wa vyanzo vitano vya habari , majeruhi wamesafirishwa kutoka nchini Syria katika siku chache zilizopita na kupelekwa kwenye hospitali nne za kijeshi nchini Urusi.
Hali za majeruhi ni mbaya
Daktari wa kijeshi anayefanya kazi katika hospitali ya kijeshi mjini Moscow na ambaye alihusika moja kwa moja na matibabu ya waliorejeshwa kutoka nchini Syria amesema kufikia Jumamosi iliyopita kulikuwa na wagonjwa zaidi ya 50 katika hospitali anayofanya kazi huku asilimia 30 hali zao zikiwa ni mbaya .
Daktari huyo aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina kwasababu haruhusiwi kuzungumzia taarifa hizo amesema kiasi cha ndege tatu zilizokuwa zimewabeba majeruhi wapiganaji zilitua mjini Moscow kati ya Ijumaa na Jumatatu asubuhi wiki hii.
Amesema walirejeshwa kwa kutumia ndege maalumu za mizigo zenye vifaa maalumu vya kitabibu kwa ajili ya kutoa huduma za dharula ambazo zilikuwa na majeruhi kadhaa.
Maria Zakhrova msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Urusi amesema taarifa za awali zinaonesha kuwa raia watano wa Urusi wanaweza kuwa wameuawa katika uwanja wa mapambano lakini hawakuwa wanajeshi wa Urusi na kusisitiza kuwa taarifa kwamba makumi au mamia wameuawa ni taarifa za kupotosha ambazo zinatolewa na wapinzani wa Urusi.
Wizara ya ulinzi ya Urusi haikujibu maswali ya shirika la habari la Reuters kuhusiana na idadi ya waliouawa nchini Syria na msemaji wa ikulu ya Urusi , Kremlin alipoulizwa kuhusiana na vifo hivyo alisema hana la kuongeza tofauti na taarifa za awali.
Ikuru ya Urusi imesema mapema wiki hii kuwa haina taarifa zozote kuhusiana na vifo hivyo.
Shirika la habari la Reuters halikufanikiwa kufanya mawasiliano ya moja kwa moja na waajiri wa wakandarasi hao wa ulinzi, kampuni ijulikanayo kama "Wagner Group" ambao wapiganaji wake wamewahi katika siku zilizopita kupokea medali kutoka ikulu ya Kremlin.
Daktari wa kijeshi amesema daktari mwenzie aliyekwenda nchini Syria hivi karibuni alimueleza kuwa kiasi ya watu 100 katika jeshi la Urusi wameuawa katika kipindi cha wiki iliyopita na wengine 200 wamejeruhiwa.
Mwandishi : Isaac Gamba/rtre
Mhariri: Iddi Ssessanga