1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapiganaji wa Yemen wadhibiti eneo karibu na makazi ya rais

Isaac Gamba
31 Januari 2018

Wapiganaji wa  Yemen wanaotaka kujitenga wanaoungwa mkono na Umoja wa Falme za Kiarabu hapo jana wamedhibiti eneo jirani na makazi ya rais katika mji wa kusini wa  Aden.

https://p.dw.com/p/2roS6
Sicherheitskräfte Polizei in Aden Jemen
Picha: Getty Images/AFP

Muungano wa kijeshi  unaoongozwa na Saudi Arabia ambao pia unaundwa na Umoja wa Falme za Kiarabu  umekuwa ukipambana na waasi kaskazini mwa Yemen kwa karibu miaka mitatu kwa niaba ya serikali ya  rais Abed Rabbo Mansour Hadi lakini licha ya hilo , Umoja wa Falme za Kiarabu  pamoja na serikali ya Hadi wamekuwa wakivutana wenyewe kwa wenyewe kudhibiti madaraka ya serikali ya  nchi hiyo mapambano ambayo yalishika kasi mwishoni mwa wiki.

Kwingineko nchini Yemen wanamgambo wa al-Qaida walishambulia kituo cha ukaguzi barabarani katika jimbo la kusini la Shabwa na kuwaua kiasi ya wanajeshi 12 katika eneo ambalo wanajeshi wa Yemeni awali  walitangaza ushindi dhidi ya wanamgambo hao.

Katika taarifa ya wanamgambo hao iliyosambazwa kupitia  mitandao ya kijamii walidai  shambulizi hilo lilikuwa ni kulipiza kisasi dhidi ya vikosi vinavyoungwa mkono na Marekani  na Umoja wa Falme za Kiarabu.

Maafisa wa usalama wamesema wapiganaji tiifu kwa kundi linalotaka kujitenga  walifanya mashambulizi katika maeneo jirani na lango la makazi ya rais mjini Aden  na kusababisha wanajeshi tiifu kwa Abed Mansour Hadi kulazimika kuondoka kwenye  maeneo yao.

 

Waziri Mkuu wa serikali ya Hadi atakiwa kuondoka

Jemen Präsident Abed Rabbo Mansur Hadi
Rais wa Yemeni Abed Rabbo Mansur HadiPicha: Reuters/F. Al Nasser

Maafisa hao wamesema Waziri Mkuu wa serikali ya Hadi pamoja na mawaziri kadhaa  wanatarajiwa kuondoka Yemeni kwenda Riyadh ambako ndiko aliko Hadi lakini hadi jana  Jumanne jioni ilikuwa haijafahamika wazi iwapo tayari wameondoka.

Hata hivyo wapiganaji wa majeshi ya muungano unaoongozwa na Saudi Arabia ambao wamekuwa wakidhibiti ulinzi wa makazi hayo ya rais waliwazuia wapiganaji wa upande unaotaka kujitenga wasiingie katika lango la makazi hayo.

Maafisa hao waliozungumza kwa sharti la kutotaja majina wamelieleza shirika la Associated Press kuwa Waziri Mkuu Ahmed Obaid Bin Daghar  na mawaziri kadhaa bado wako katika makazi hayo.

Katika mkoa wa kaskazini wa Dar Saad, walioshuhudia wanasema ndege za majeshi ya muungano unaoongozwa na Saudi Arabia zilishambulia kambi ya kijeshi ya vikosi tiifu kwa Hadi  kabla ya wapiganaji wa upande unaotaka kujitenga  kudhibiti eneo hilo.

Brigedia Jenerali  Mahran al-Qubati alilieleza shirika la habari la AP kuwa vikosi vyake vinaheshimu hatua ya usitishaji mapigano iliyotangazwa mapema hapo jana  na majeshi ya muungano unaoongozwa na Saudi Arabia lakini hata hivyo wapiganaji wanaotaka kujitenga walitumia fursa hiyo  kushambulia kambi yake ingawa Kanali Turki al- Malki msemaji wa majeshi ya muungano unaoongozwa na Saudi Arabia alikataa kuzungumzia shambulizi hilo na kusema hayuko tayari kuzungumzia operesheni hiyo.

Mapigano hayo yalizuka Jumapili mjini Aden baada ya muda uliowekwa na upande unaotaka kujitenga  kwa serikali kutakiwa kuwa imejiuzulu kumalizika huku  Abed Rabbo  Mansour Hadi ambaye amekuwa Saudi Arabia katika kipindi chote cha mapigano nchini Yemen  akisema hatua iliyochukuliwa na upande unaotaka kujitenga ni sawa na mapinduzi.

Kwa mujibu wa shirika la kimataifa la Msalaba Mwekundu mapigano hayo hadi sasa yamewaua kiasi watu 36 na kuwajeruhi wengine 185 tangu yalipoanza Jumapili.

Mwandishi: Isaac Gamba/ape

Mhariri      :Yusuf Saumu