Wapiganaji Somalia 'kuyalinda' mashirika ya misaada
24 Julai 2008Kiongozi mpya wa upande wa upinzani nchini Somalia,Sheikh Hassan Dahir Aweys ameapa kuwalinda watumishi wa mashirika yanayotoa misaada katika taifa hilo la pembe ya Afrika.
Hali mbaya ya kiusalama ilioko huko imeyazuia mashirika kadhaa ya kimisaada kuendelea na kazi zake huko huku wananchi wengi wakiteseka wakiwa hawana mahitaji muhimu kama vile chakula na malazi kutokana na vita pamoja na ukame .
Kauli ya kiongozi huyo wa ushirika wa kuikomboa tena Somalia ARS alioko uhamishoni nchini Eritrea,imekuja baada ya mashirika mengi ya utoaji misaada kusimamisha shughuli zake kufuatia visa vya kuuliwa kwa watumishi wake.Umoja wa Mataifa unasema kuwa jumla ya watumishi wa shughuli za kutoa misaada 19 wameuawa mwaka huu huku wengine 13 kuchukuliwa mateka.
Pia imekuja wakati Umoja wa mataifa kutoa onyo kuwa mauaji pamoja na utekaji nyara wa watumishi wa mashirika ya misaada nchini Somalia kunatishia kuvuruga juhudi za kujaribu kulipatia ufumbuzi janga la kibinadamu ambalo linachukuliwa kama baya zaidi duniani. Takriban wasomali millioni 2 Unusu hawana chakula kutokana na hali mbaya na pia Umoja wa mataifa unaonya kuwa ifikapo mwisho wa mwaka huu idadi yao itafikia millioni 3 Unusu.
Aidha kiongozi huyo Aweys ,ambae ameorodheshwa kama gaidi na Marekani pamoja na Umoja wa mataifa, amewasifu watumishi hao kwa kazi yao huku akiomba msaada zaidi kwa kundi lake ili kuyafurusha majeshi ya Ethiopia kutoka nchini mwake.
Majeshi ya Ethiopia yanapambana vikali dhidi ya wapiganaji wa kiislamu wanaoendesha hujuma za ushambulizi wa hapa na pale huku wakijificha.Na taarifa zaidi kutoka huko zikiwanukuu walioshuhudia, zinaeleza kuwa vikosi vya Ethiopia leo alhamisi vimewauwa raia tisa katikati mwa nchi hiyo baada ya vikosi hivyo kushambuliwa na wapiganaji wa chini kwa chini.
Taarifa zaidi zinasema kuwa vikosi hivyo vilishambuliwa wakati vinarejea katika kambi ya mji wa Beledewyne, ulioko umbali wa kilomita 350 kaskazini ya mji mkuu wa Mogadishu.Na baada ya kushambuliwa vilijibiza kwa kuwafyatulia risasi raia.
Ethiopia ilituma vikosi vyake nchini Somalia mwaka wa 2006 kusaidia kuuondoa madarakani utawala wa mahakama za kiislamu.Wapiganaji wa kiislamu wameapa kupigana hadi mtu wa mwisho ili kuwaondoa askri hao kutoka ardhi ya Somalia.
Katika harakati nyingi za wapiganaji hao wamekuwa wakiwauwa na kuwateka nyara watumishi wa mashirika yanayotoa misaada.
Lakini jana jumanne kiongozi mpya wa kundi hilo la the Alliance for the Re-Liberation of Somalia ARS,Sheikh Hassan Dahir Aweys,akizungumza kwa simu na shirika la habari la Reuters kutokea Eritrea, alisema kuwa analaani vitendo hivyo ,akiongeza kuwa anashukuru kazi yao ngumu na ya maana ya kusaidia jamii ya wasomali inayotaabika kutokana na ukosefu wa chakula.
Aweys amechukua uongozi wa kundi hilo baada ya kiongozi wake wa zamani mwenye msimamo wa kadiri,Sheikh Sharif Ahmed pamoja na wanachama wengine 36, kufukuzwa kutoka chama hicho kutokana na hatua yao ya kutia saini mpango maalum na serikali ya mpito ya Somalia nchini Djibout mwezi uliopita.
Miongoni mwa mengine mpango huo unagusia ratiba maalum ya kuondoka kwa majeshi ya Ethiopia na mahali pake kuchukuliwa na kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa mataifa.