Wapiga kura wengi wajitokeza katika uchaguzi wa Uholanzi
15 Machi 2017
Wakati uchaguzi wa bunge nchini Uholanzi ukitarajiwa kukamilika, waziri mkuu wa nchi hiyo Mark Rutte wa chama cha VVD ametajwa kuwa mbele ya mpinzani wake mkuu Geerd Wilders wa chama cha ukombozi PVV kinachoendeleza siasa za mrengo wa kulia. Hayo ni kwa mujibu wa mtandao unaojumuisha matokeo ya kura za maoni za mashirika ya utafiti.
Kwa mujibu wa mashirika ya kuendesha tafiti za maoni, dalili zimeonesha kuwa idadi kubwa ya wapiga kura wamejitokeza vituoni kupiga kura nchini Uholanzi katika uchaguzi ulioanza alfajiri na utakamilika saa tatu usiku. Saa tatu baada ya vituo kufunguliwa, takriban asilimia 33 ya wapiga kura walishajitokeza, tofauti na asilimia 27 waliojitokeza muda sawa na huo katika uchaguzi uliopita mwaka 2012.
Waziri Mkuu Mark Rutte aliwashauri wapigaji kura milioni 13 kushiriki kwenye shughuli hiyo muhimu. Rutte amesema "huu ni uchaguzi wa tatu baada ya Brexit na Marekani. Tuna chaguzi zinazokuja za Ufaransa na Ujerumani, na hii ni nafasi kwa nchi kubwa yenye demokrasia kama Uholanzi kupitisha ujumbe wa kukomesha fikra potovu za siasa kali za kizalendo na bado kuna kitisho cha kuamka Alhamisi na kushuhudia Geert Wilders anaongoza chama kikubwa."
Utabiri wa PVV kupoteza uungwaji mkono
Kwa mujibu wa utabiri wa mtandao wa Peilingwijzer unaojumuisha matokeo ya kura za maoni kutoka kwa mashirika yanayokusanya maoni, chama cha Waziri Mkuu Mark Rutte kitapata kati ya viti 24 na 28 vya bunge miongoni mwa jumla ya viti 150 vinavyowaniwa. Chama cha kizalendo cha siasa kali za mrengo wa kulia kinachoongozwa na Geert Wilders kinatarajiwa kupata kati ya viti 19-23. Hata hivyo Wilders ambaye kampeni zake zimekuwa dhidi ya wakimbizi na kutaka kuondoa uislamu nchini humo, amepuuzilia mbali kura hiyo ya maoni ya hivi punde kuwa chama chake kinapoteza uungwaji mkono.
Uchaguzi wa Uholanzi unaofanyika kabla uchaguzi wa Ufaransa na Ujerumani mwaka huu, unatizamwa kuwa kipimo cha ushawishi wa vyama vya siasa kali za kizalendo barani Ulaya, vinavyopinga wakimbizi na Uislamu, ikizingatiwa nchi hizo pia zinavyo vyama vinavyounga mkono sera sawa na hizo.
Matokeo ya awali yanatarajiwa kuanza kutangazwa baada ya vituo kufungwa saa tatu usiku na yataashiria jinsi bunge jipya litakavyokuwa. Matokeo rasmi yatatangazwa wiki ijayo.
Uchaguzi wa Uholanzi unafanyika wakati nchi hiyo imegubikwa kwenye mgogoro wa kidiplomasia na Uturuki. Hapo jana rais wa uturuki Recep Tayyip Erdogan alilaumu Uholanzi kwa kuwaua wanaume na wavulana wa kiislamu 8,000 wa Bosnia katika mauaji ya kimbari ya mwaka 1995 yaitwayo Srebrenica yaliyofanywa na vikosi vya Serb cha Bosnia.
Mwandishi: John Juma/DPAE/APE
Mhariri: Yusuf Saumu