Wapiga kura wengi kujitokeza uchaguzi wa Mali
25 Julai 2013Msemaji wa wizara ya mambo ya ndani ya Mali, Gamer Dicko, amesema nchi hiyo ina historia ya chaguzi mbaya, lakini uchaguzi wa Jumapili utakuwa tofauti. Idadi ya watu waliochukua kadi za kupigia kura imepita makadirio na sasa imefikia asilimia 82. "Hii inaashiria tunaweza kuwa na matumaini ya kuwa na rekodi ya watu watakaoshiriki zoezi la upigaji kura. Katika chaguzi zilizopita, hatujawahi kuwa na zaidi ya asilimia 66 ya kadi za kura kuchukuliwa," ameongeza kusema waziri Dicko.
Naibu wa kwanza wa mwenyekiti wa tume ya uchaguzi ya Mali, Issaga Kampo, amesema kama kadi nyingi za kura zitawafikia wenyewe, basi bila shaka watu wengi watajitokeza kupiga kura. "Zaidi ya asilimia 70 ya kadi za kupigia kura zimeshawafikia wenyewe. Katika baadhi ya vitongoji tumefanikiwa kuwafikia asilimia 100 ya waliojisajili na tumewapa kadi zao. Natarajia wapigaji kura zaidi ya asilimia 50 kujitokeza."
Jumuiya ya kimataifa iliishinikiza Mali kuandaa uchaguzi Julai 26 mwaka huu kuhakikisha nchi inarejea katika utawala wa kikatiba kabla kupokea dola bilioni 4.3 kama msaada wa maendeleo na ujenzi mpya wa taifa hilo.
Wakimbizi huenda wasipige kura
Licha ya kuwepo matumaini ya wapigaji kura kujitokeza kwa wingi, Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshuhulikia masuala ya wakimbizi, António Guterres, ameelezea wasiwasi wake kuhusu uwezo wa wakimbizi wa ndani na nje ya nchi, zaidi ya nusu milioni raia wa Mali kupiga kura zao siku ya uchaguzi. Kaimu mjumbe wa shirika hilo kwa ajili ya Mali, Sebastien Apatita, amesema kadi 300 pekee za kura zimewafikia wakimbizi wa Mali nchini Niger, Burkina Faso na Mauritania, ingawa takriban 11,000 kati yao walitambuliwa kwenye daftari la wapiga kura. Apatita aidha amesema hali hiyo hiyo inawakabili pia watu waliolazimika kuyahama makazi yao.
Tume ya uchaguzi ya Mali ina wasiwasi mapungufu katika daftari la majina ya wapigaji kura huenda yakatumiwa na wagombea watakaoshindwa, kuweka mazingira ya kutokea vurugu baada ya uchaguzi wa Jumapili. Tume hiyo inakadiria wapigaji kura milioni 1.1 hawakusajiliwa. Miongoni mwao ni vijana 300,000 wenye umri kati ya miaka 18 na 20, ambao hawakuwa wametimiza umri unaotakikana kisheria wakati mchakato wa kuwasajili wapigaji kura ulipofanyika kati ya mwaka 2009 na 2011.
Kinyang'nyiro kikali
Wagombea 27, wakiwemo mawaziri wakuu watatu wa zamani na mwanamke mmoja, wanashindana kuiongoza Mali kwa miaka mitano ijayo katika uchaguzi ambao umewaacha maelfu ya raia wa Mali wakiwa wamenyima haki yao ya kuchagua kiongozi wanayemtaka. Wanaopigiwa upatu kushinda ni wale wenye fedha nyingi, wanaoaminiwa kuwa mawaziri wakuu wa zamani, Ibrahim Boubacar Keita, Soumaila Cisse, Soumana Sacko na waziri wa zamani wa fedha, Cheikh Modibo Diarra.
Mgombea pekee mwanamke, Haidara Cisse, anayeungwa mkono na makundi mengi ya wanawake yenye ushawishi mkubwa nchini, anatarajiwa kufanya vizuri katika uchaguzi huo. Mgombea mwingine, Tiebele Drama, alijiondoa katika kinyang'anyiro cha Jumapili kutokana na wasiwasi juu ya kuwepo haki katika mchakato mzima wa uchaguzi huko mji wa kaskazini wa Kidal, ambao licha ya mkataba wa muda wa amani, unabakia kukaliwa na waasi wa Tuareg.
Wasiwasi mkubwa kuhusu usalama bado ungalipo katika vituo vyote vya kupigia kura, hususan katika miji ya kaskazini ya Timbuktu na Gao, ambako kuna idadi kubwa ya wanajeshi wa Mali.
Mwandishi: Josephat Charo/DPAE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman