1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapiga kura Bukavu wapoteza kadi zao

Mitima Delachance19 Desemba 2018

Maelfu ya watu katika eneo la Bukavu, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, watakuwa na shida ya kuweza kupiga kura Jumapili Desemba 23 kwa sababu walizipoteza kwa muda mrefu.

https://p.dw.com/p/3AMqP
Demokratische Republik Kongo Wahlkampagne Felix Antoine Tshilombo Tshisekedi in Bukavu
Picha: Lydie Omanga

Siku nne kabla ya uchaguzi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo huenda maelfu ya watu nchini humo watakuwa na shida ya kuweza kupiga kura Jumapili Desemba 23 kwa sababu hawana kadi za wapiga kura walizopoteza kwa muda mrefu. Leo hii wameandamana mbele ya ofisi za Tume Huru ya Uchaguzi, CENI, wakisisitiza kwamba kila mara wanaomba kadi kutoka tume hiyo bila mafanikio, huku muda unasonga.

Tangu mwanzo wa wiki hii ya mwisho kabla ya uchaguzi nchini humu. Umati wa wakaazi wa Bukavu waliozipoteza kadi zao zitakazowawezesha kupigakura na ambazo pia zinatumikishwa kama vitambulisho vyao, wanafika kwa wingi mbele ya ofisi ya CENI mjini Bukavu, ili kuomba kadi nyingine au "duplicata."

Emmanuel Ramazani Shadary ni mgombea wa urais wa chama tawala
Emmanuel Ramazani Shadary ni mgombea wa urais wa chama tawalaPicha: Getty Images/AFP/J. Wessels

Wengi wao wanasema kuwa wamezipoteza katika njia tofauti ikiwemo kuibiwa, na hasa zaidi wale waliopoteza kadi zao wakati wa kuteketea kwa nyumba zaidi ya mia tano mjini Bukavu kati ya Juni na Septemba mwaka huu. Watu hao wanasema wamerudishwa kwenye ofisi hii mara nyingi bila kufanikiwa kuzipata kadi hizo.

Wengine wanashangazwa kwa sababu waliambiwa kwamba watapewa kadi hizo Jumatatu Desemba 24, wakati ambapo uchaguzi utafanyika Jumapili Desemba 23:

Ofisi ya CENI inayohusika na kuzigawa kadi hizo kwa wapigakura imeiambia DW kwamba ina kompyuta moja tu inayotumika kutoa kadi hizo na kwamba kompyuta hii ina uwezo wa kufyatua kadi themanini na tatu tu kwa siku, isipokuwa izimwe kwa muda wa masaa mawili na iwashwe baadaye kwa kuzifyatua kadi zingine, ijapokuwa kuna watu yapata elfu saba wanaosubiri, mji wa Bukavu ukiwa na zaidi ya watu milioni moja.

Umoja wa Mataifa umewataka Wakongomani kuzingatia utulivu wakati wa uchaguzi.
Umoja wa Mataifa umewataka Wakongomani kuzingatia utulivu wakati wa uchaguzi.Picha: Reuters/S. Mambo

Wakaazi wengine wanapendekeza kwamba ikiwa tume ya uchaguzi itashindwa kuwahudumia kwa wakati, iwape angalau vikaratasi vitakavyowarahisishia kupiga kura siku ya Jumapili. La sivyo, hawata piga kura.

Uongozi wa tume ya uchaguzi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo haujajibu ombi hilo.

Mwandishi: Mitima Delachance/DW Bukavu
Mhariri: Mohammed Khelef