Wapambanao na Ebola washambuliwa DRC
23 Oktoba 2018Daktari Ndjokolo Tambwe Bathe, ambaye alizungumza na wanahabari siku ya Jumanne (23 Oktoba) baada ya mashambulizi mabaya ya waasi na maandamano mwishoni mwa wiki, alisema wafanyakazi wawili wa afya waliuliwa na waasi hao.
Siku iliyofuatia, wakaazi wa mji wa Beni waliandamana kulalamikia shambulio jingine ambalo lilisababisha watu 15 kuuawa; na magari pamoja na makundi ya wahudumu wa afya kupigwa mawe.
Aidha mamia ya watoto walitekwa nyara suala ambalo limechangia kusitishwa kwa juhudi za kukabili maambukizi ya virusi hivyo vya Ebola.
Naibu Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterress, Farhan Haq, amesema Guterress ameghadhabishwa na mashambulio dhidi ya wahudumu wa afya, na kuyataka makundi yote yaliyojihami kusitisha mashambulizi hayo.
"Katibu Mkuu amekasirishwa na mauaji na kutekwa kwa raia na makundi yaliyojihami katika eneo la Beni, Kivu Kaskazini, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Analaani mauaji ya siku ya Jumamosi ambapo raia 15, akiwemo mvulana mmoja, waliuawa, pamoja na kujeruhiwa na kutekwa nyara kwa wengine wengi wakati wa shambulizi lililofanywa katika mji wa Mayongose, kwenye viunga vya mji wa Beni."
Mjumbe wa Shirika la Afya Duniani kuhusu masuala ya Ebola katika mkoa wa Kivu Kaskazini, Dkt. Michel Yao, aliliambia shirika la habari la AP kwamba juhudi za kimatibabu zilikuwa zimeanza kuonesha matokeo mazuri lakini shambulizi hilo jipya lingelizirejesha nyuma hatua zilizopigwa kufikia wakati huo.
"Kila mara juhudi za kukabili Ebola zinapositishwa, shughuli za utoaji wa chanjo na kuwatambua walioathirika zinaathiriwa," alisema Daktari Ndjokolo Bathe, anayeshiriki kwenye kampeni dhidi ya ugonjwa huo, akisikitikia hali hiyo na kuonya kuwa wakaazi walikuwa wanajiweka katika hatari.
Bathe alisema siku kadhaa zilizopita, kundi moja la vijana mjini Beni liliuiba mwili wa mwathiriwa wa Ebola ulipokuwa ukisafirishwa kwenda kuzikwa, baada ya familia ya marehemu kuwakubalia.
"Baada ya kuushika mwili wake, mmoja wa vijana hao aliambukizwa virusi hivyo na kufariki."
Mwandishi: Sophia Chinyezi/APE
Mhariri: Iddi Sessanga